Header Ads Widget

UPELELEZI KESI YA UHUJUMU UCHUMI KCBL WAKAMILIKA....

 Na Gift Mongi MATUKIO DAIMA APP,Moshi.

Upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili waliokuwa wafanyakazi watatu wa benki ya Ushirika ya Kilimanjaro(KCBL)  umekamilika huku upande wa mashitaka ukiwasilisha mahakamani mashahidi 29 na vielelezo vipatavyo 471.


Katika kesi hiyo  namba 5 ya mwaka 2023 ilikuwa ikisikilizwa na Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi Moshi,  Salome Mshasha huku upande wa mashitaka ukiongozwa na Mawakili wa serikali Donasian Chuwa, Samwel Kaaya, Henry Kasiano Daudi na Bora Msafiri Mfinanga.


Itakumbukwa kuwa mnamo Octoba 2019,  Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro   iliwafikisha katika mahakama ya hakimu mkazi Moshi,  Joseph  Kingazi,  na Elizabeth Makwabe  wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali ikiwemo uhujumu uchumi na baadaye Juni,  2021 aliyekuwa mhasibu wa benki hiyo, Ombeni Masaidi aliunganishwa katika kesi hiyo.


Washitakiwa hao kwa pamoja walikuwa wanashitakiwa kwa makosa 13, ikiwemo makosa 9 ya kughushi na kutoa nyaraka za uongo, kosa moja la kuongoza uhalifu wa kupanga, kosa moja la ubadhirifu wa fedha za umma na  kuisababishia mamlaka hasara ya  zaidi ya Sh2.4 bilioni.


Akisoma maelezo ya mashahidi(Commital proceedings)  Mwendesha mashitaka wa serikali, Donasian Chuwa, mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Salome Mshasha alieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.


"Katika usikilizwaji wa kesi hii ya uhujumu uchumi ambayo upelelezi wake umekamilika, upande wa mashitaka  tukatakuwa na mashahidi 29 pamoja na vielelezo 471,"Wakili Chuwa aliieleza mahakama hiyo


Hata hivyo, baada ya upande wa mashitaka kuwasilisha maelezo hayo, Hakimu Mshasha aliwaeleza washitakiwa hao kuwa, kwa kuwa mahakama imewafahamisha na kusikia idadi ya mashahidi pamoja na vielelzo vitakavyotumika wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo katika mahakama kuu Divisheni ya uhujumu uchumi, chochote watakachokisema mbele ya mahakama hiyo kitatumika kama ushahidi wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.


Hivyo washitakiwa hao kwa pamoja, walimweleza hakimu Mshasha kuwa watakuwa na mashahidi wao pamoja na vielelezo vyao.


Hakimu Mshasha aliwaleza washitakiwa hao kuwa wataendelea na dhamana yao mpaka hapo watakapopewa taarifa rasmi juu ya usikilizwaji wa kesi hiyo


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI