Header Ads Widget

SERIKALI YAKAMILISHA UKARABATI MT SANGARA

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma


SERIKALI imekamilisha ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT Sangara ambayo itaanza majaribio karibuni ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa nchi zilizo mwambao wa ziwa Tanganyika.

 


Mhandisi Mkuu wa meli ya MT Sangara, David  Jenga akitoa taarifa kwa kamati ya siasa ya Halmashauri kuu ya CCM mkoa Kigoma ilipofanya ziara kukagua maendeleo ya ukarabati huo alisema kuwa ukarabati huo umeongeza utendaji wa meli hiyo kwa kiwango kikubwa.



Meli hiyo inatarajia kuanza kazi wakati wowote baada ya miezi 14 ya ukarabati mkubwa uliogharimu kiasi cha shilingi Bilioni nane ukarabati ambao utaongeza ufanisi mkubwa kiutendaji wa meli hiyo sambamba na kuongeza mapato ya serikali.



Jenga alisema kuwa ukarabati huo unahusisha uwekaji wa  injini mpya,kubadilisha matanki ya kutunzia mafuta, mifumo ya usukani, pampu na mabomba ya kushushia mafuta ambapo ukarabati huo umewezesha kuongeza uwezo wa pampu kupakua mafuta kutoka masaa 72 hadi kufikia masaa manane huku injini ikiwa na uwezo wa kutembea masaa matano kutoka Kigoma hadi Bandari ya Kalemie Congo kutoka masaa 24 ya awali.



Akizungumzia ukarabati huo Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Abdulkadri Mushi amepongeza serikali kwa ukarabati wa meli hiyo kwa usimamizi wa kampuni ya huduma za meli (MSL) na kwamba ukarabati huo unatija kubwa katika kutoa huduma lakini pia kuongeza mapato ya serikali.



Pamoja na pongezi hizo Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi wilaya ya Kigoma, Juma Chaurembo ameiomba serikali kuharakisha ukarabati wa meli ya Mv.Liemba kwani ina maslahi makubwa ya mzunguko wa uchumi wa wananchi wa mkoa Kigoma na kutofanya kazi kwake kumeathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa watu wengi mkoani Kigoma.

 



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI