NA WILLIUM PAUL, SIHA.
VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake kuanzia ngazi ya Matawi, Kata, Wilaya na Mkoa wametakiwa kutotumia nafasi walizonazo kuwaumiza wananchi na badala yake watumike kuwasaidia ili kuondokana na matatizo yanayowakabili.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu wa Siasa na Oganizesheni Jumuiya ya Wazazi Taifa, Said King’eng’ena wakati akitoa mafunzo kwa viongozi wa chama na Jumuiya zake ngazi ya matawi, kata na Wilaya katika wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
King’eng’ena alisema kuwa, jukumu la chama cha Mapinduzi ni kuwatumikia wananchi katika kuwaletea maendeleo na sio kutumia nafasi mbalimbali kuwanyanyapa na kuwanyanyasa.
“Wapo baadhi ya watu baada ya kupata uongozi mmeanza kupandisha mabega na kusahau wajibu wenu wa kuwatumikia wananchi mnapaswa kutambua jukumu la kiongozi ni kuwatumikia wananchi na kuwasaidia kumaliza matatizo yanayowakabili” alisema King’eng’ena.
Katibu huyo wa Oganizesheni alisema kuwa, wanachama wa Chama cha Mapinduzi wanaimani kubwa na viongozi wake na ndio maana wamekuwa wakiwachagua katika nafasi mbalimbali za uongozi katika chama na Serikali hivyo kila kiongozi anawajibu wa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo.
Alisema kuwa, Kiongozi anawajibu wa kuonyesha njia na heshima kwa wale anaowaongoza na kuwataka viongozi wanaotokana na chama cha Mapinduzi kuwa mfano wa kuingwa katika jamii.
“Viongozi mnawajibu wa kutosheka na mlichonacho wapo baadhi yetu mmekuwa mkitumia nafasi mlizopewa na wanachama kujipatia fedha kinyume na sheria kiongozi wa staili hii hafai katika jamii na hili linapelekea baadhi ya watu kuchukia chama chetu kutokana na uonevu huu sasa mnapaswa kubadilika” alisema King’eng’ena.
Aidha aliwataka viongozi kujijengea tabia ya kuacha alama nzuri katika uongozi wao ili pindi wanapomaliza muda wao wananchi wawakumbuke kutokana na mazuri ambayo ameyafanya katika kipindi cha uongozi wake.
Kiongozi huyo pia aliwaasa viongozi hao kuwa na tabia ya kutunza siri za vikao pamoja na kukosoana kwa kufuata taratibu za chama kupitia vikao maalum na sio kuchafuana kwa wananchi.
Mwisho…
0 Comments