Header Ads Widget

PROF. MKENDA ASISITIZA USHIRIKIANO NA WADAU KUTEKELEZA MAGEUZI YA ELIMU.


 

Na Mbaruku Yusuph,Matukio Daima APP Tnga 

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amezitaka Taasisi za Dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali  mbalimbali wanaotoa huduma za Elimu na wadau wengine kushirikiana na serikali kutekeleza mageuzi ya elimu.


Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Julai 12, 2023 akizindua Mradi wa uboreshaji wa shule ya Sekondari ya Mapatano iliyopo Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga unatekelezwa na Taasisi ya_Abbort Fund_.


Akifafanua zaidi kuhusu mageuzi hayo tarajiwa Prof. Mkenda amesema mfumo wa Elimu utakuwa na Mabadiliko makubwa yanayolenga kutoa elimu ujuzi.


"Huko mbele ya safari, Elimu ya lazima itakuwa ni miaka kumi na pengine tukichanganya na Elimu ya Awali itakuwa kumi na moja na Elimu ya Sekondari kutakuwa na mikondo miwili mkondo wa elimu ya jumla, ambapo mtoto atasoma kidato cha Kwanza mpaka cha Nne, yakihusisha masomo ya darasani na mafunzo kwa vitendo na  mkondo wa Amali ambao utahusisha masomo machache ya Jumla  na mafunzo ya amali  mfano ufundi, kilimo, uvuvi, michezo Sanaa na kadhalika . Alifafanua Prof. Mkenda.


Ameongeza kuwa mwelekeo wa serikali katika mageuzi ya Elimu yanayokuja jamii inapaswa kufahamu dhana nzima ili kuipa msukumo wa kila mmoja kushiriki na hatimae  kuleta matokeo chanya ya kutoa wahitimu wenye ujuzi.


Awali akitoa taarifa ya mradi wa kuboresha Shule ya Sekondari Mapatano Rais wa Abbott Fund Bi. Mellisa Brotz amesema wanazitambua juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika nyanja mbalimbali za Kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuboresha mageuzi ya elimu, uboreshaji miundombinu ili kuwezesha upatikanaji wa Elimu Bora kwa Watanzania hivyo wanaendelea kuunga mkono juhudi hizo.


Bi. Brotz ameeleza uboreshaji katika shule hiyo utahusisha ujenzi wa madarasa mapya, ukarabati wa madarasa yaliyopo, ujenzi wa mabweni ya Wasichana pamoja na nyumba za walimu.


Aidha ameongeza kuwa  mradi pia utajumuisha ujenzi wa bwalo la chakula, kituo cha huduma ya kwanza na miundombinu ya michezo.


Kwa mujibu wa Mshauri elekezi wa Mradi huo, Msanifu Majengo David Kibebe, amemhakikishia Waziri kuwa mradi huo utakamilika Julai, 2024 kwani tayari Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kuanza utekelezaji.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI