Header Ads Widget

PROF. MKENDA ASISITIZA TAASISI ELIMU YA JUU KUFANYA MAPITIO YA MITAALA.

 



Na Mbaruku Yusuph,Matukio Daima APP Tanga.


TAASISI za Elimu ya juu Nchini zimetakiwa kufanya mapitio ya Mitaala ya elimu iliyopo kwa kuzingatia miongozo ili kuendana na mabadiliko ya soko la Ajira.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda Julai 18, 2023 wakati akizindua rasmi Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo Kukuza Ujuzi Nchini Kupitia Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia kwa Uchumi Imara na Shindani



Prof Mkenda alisema kauli mbinu ya Maonesho hayo inaakisi hali halisi na matarajio ya Watanzania na  Taifa litaendelea na mchakato wa mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na Mitaala ya Elimu na Mafunzo kwa ngazi zote.


Alisema Serikali inatambua kuwa Elimu ya Juu ni Elimu ya Kimataifa, kwa kuzingatia hilo amevisisitiza Vyuo Vikuu kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali duniani ili kujenga mahusiano yenye tija kuwawezesha Watanzania kupata maarifa na ujuzi.


"Leo tumeweka sahihi ya mashirikiano ya kielimu kati ya Tanzania na Serikali ya Hungary, ambapo kutakuwa na ufadhili wa Wanafunzi kwenda kusoma nchi hiyo, vile vile Tanzania itatoa ufadhili wa Wanafunzi wao kuja kusoma hapa nchini, ili kuvifanya Vyuo Vyetu kuwa vya Kimataifa kwa kupokea wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali duniani, na hatimae kutoa wahitimu wenye Ujuzi na stadi za maisha " alieleza Prof. Mkenda.



Mbali na hayo pia Prof. Mkenda amezitaka Taasisi hizo kuhakikisha zina buni program mpya zitakazoendana na wakati pamoja na kuimarisha au kuanzisha mahusiano yenye tija baina yake na Taasisi za utafiti pamoja na sekta binafsi na kuweka utaratibu wa kuendeleza Teknolojia na kuhamasisha matumizi yake ili kuongeza kasi ya Maendeleo ya kijamii.


Awali akizungumza kuhusu Maonesho hayo, Mkurugenzi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof. Charles Kihampa amesema jumla ya Taasisi 83 za ndani na Nje ya nchi zimeshiriki ukilinganisha na Taasisi 75 zilizoshiriki Maonesho kwa mwaka uliopita.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI