NA WILLIUM PAUL, SAME.
NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga amewaonya watu wanaombeza na kumtukana Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kuacha mara moja.
Naibu Waziri Ummy alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na vikundi vya wakinamama katika wilaya ya Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro ambapo alisema kuwa, Rais amekuwa akiwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo ambapo ndio hitaji lao.
"Wapo watu ambao wamekuwa wakizalilisha Rais wetu kwa maneno ya kejeli na kumtukana sasa nitumie nafasi hii kuwaonya kuachana na hiyo tabia kwani Watanzania hatupo tayari kuona Rais wetu akichafuliwa hovyo" alisema Naibu Waziri Ummy.
Alisema kuwa, Rais Dkt Samia kupitia Serikali yake ya awamu ya sita ametoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi kuilinda na kuitunza miradi hiyo na kuwapuuza wale wote wanaoeneza taarifa za uongo na kumchafua.
Akizungumza swala la uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025, Naibu Waziri Ummy aliwataka wakinamama kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Alisema kuwa, wakinamama ni jeshi kubwa ambalo likiamua linaweza na kuwaomba kumbeba Rais Dkt Samia ili kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu.
"Sisi wakinamama wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi tumeshaamua tunaenda na Dkt. Samia hivyo natambua na wanawake wa Same na Mwanga tutahakikisha tunampambania kwa wananchi kwa kueleza kazi kubwa ambazo amekuwa akizifanya ili aweze kupata kura za kishindo katika wilaya na mkoa wetu" alisema Naibu Waziri Ummy.
Aidha Naibu Waziri huyo aliwataka wakinamama kutembea kifua mbele kutokana na kazi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Mwisho.
0 Comments