Header Ads Widget

JAMII YATAKIWA KUTOWANYANYAPAA WATU WENYE ULEMAVU.

 


NA WILLIUM PAUL, MWANGA.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga ameitaka jamii kutowanyanyapaa watu wenye ulemavu na badala yake wawafariji.


Naibu Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati alipozungumza na watu wenye ulemavu na kula nao chakula cha mchana katika wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.



Alisema kuwa, ulemavu sio ugonjwa hivyo ni jukumu la jamii kuwaunga mkono ili kutimiza malengo yao na kufika mbali.


"Sisi watu wenye ulemavu tunandoto zetu ambazo tunazotamani tuzifikie hivyo jamii inawajibu wa kutuunga mkono ili kuyafikia malengo hayo" alisema Naibu Waziri Ummy.



Na kuongeza "Sisi watu wenye Ulemavu, tunamshukuru sana na tunampenda Rais Dkt Samia Suluhu Hasani ,kwa kutujali na kututhamini ambapo amekuwa akitupa fursa mbalimbali tutaendelea kumuunga mkono na kusimama naye ili kuhakikisha mwaka 2025 tunampa kura za kishindo".


Aidha aliitaka jamii kuwaibua watoto wenye ulemavu ili waweze kupata Elimu  huku pia akiwata watu wenye ulemavu kutovunjika moyo kwani wanaweza kuwa katika nafasi yoyote wanayohitaji.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo alizitaka wilaya nyingine kwende kujifunza katika wilaya ya Mwanga kwa jinsi ambavyo watu wenye ulemavu wanavyopewa mstari wa mbele katika kuthaminiwa.



Awali akisoma risala kwa Naibu Waziri huyo, Katibu Shirikisho la watu wenye ulemavu wilaya Mwanga, Jeremiah Shayo alisema kuwa, katika wilaya ya Mwanga kunajumla ya watu wenye ulemavu wapatao 1341 na kwa upande wa watoto wenye ulemavu wapo 86.


Shayo alisema kuwa, watu wenye ulemavu wilaya humo wanashirikiana na Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.



"Tunaomba msaada wa kupata mdau atakayetusaidia katika upatikanaji wa viungo bandia kwa watu wenye ulemavu wa viungo kwa kuwa hili ni hitaji kubwa kwa baadhi yetu hivyo kupelekea kushindwa kutekeleza baadhi ya majukumu kwa sababu ya kukosa baadhi ya viungo muhimu vya mwili" alisema Shayo.


Aidha waliomba kupata wakalimani wa kujitolea ili kuwasaidia wenzao viziwi wanapofika katika taasisi mbalimbali za huduma za kijamii ambazo ni hospitali, shule, mahakama na polisi.


Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI