Header Ads Widget

MBUNGE ZUENA BUSHIRI AWAOMBA WANANCHI KUMUUNGA MKONO DKT SAMIA SULUHU HASANI.

 


NA WILLIUM PAUL, SAME.

WANANCHI wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hasani katika kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo na kutakiwa kuitunza na kuilinda miradi hiyo ili dhamira yake iweze kuonekana.


Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri wakati alipofanya mkutano wa hadhara wa wakinamama kata ya Makanya wilayani Same ambapo alisema kuwa, Rais Dkt Samia Suluhu Hasani amefanya kazi kubwa na ya mfano wa kuigwa katika kuwatumikia wananchi na kuwaletea maendeleo.



Alisema kuwa, fedha nyingi zimesambazwa katika maeneo mbalimbali nchini  ili kuhakikisha miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, Elimu, Afya na sekta nyingine zinawafikia wananchi kwa ukaribu.



"Wananchi mmeshuhudia awamu ya sita imeleta fedha nyingi za maendeleo katika maeneo yetu tunayoishi lengo likiwa ni kutusogezea huduma za kijamii karibu nasi sasa ni jukumu letu kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hasani na chama chake cha Mapinduzi kwa kazi kubwa na nzuri zinazofanyika" alisema Mbunge Zuena.



Mbunge huyo alisema kuwa, wapo baadhi ya watu wachache wenye nia hovu wasiopenda kuona nchi ikipiga hatua ambapo wamekuwa wakieneza habari za uongo kwa lengo la kukatisha juhudi za dhati za Rais Dkt Samia Suluhu Hasani.


Zuena aliwataka wananchi kuwapuuza watu hao wachache na kumuunga mkono kwa vitendo Dkt Samia Suluhu Hasani kwa kueleza waziwazi kazi kubwa ambazo amekwisha zifanya ili kila mmoja atambue.



Katika hatua nyingine Mbunge huyo alisema kuwa mwaka ujao ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuwaomba wakinamama kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi pamoja na kuwachagua viongozi wanaotokana na chama cha Mapinduzi.


"Katika nchi hii hakuna chama siasa kitakachoweza kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kama chama cha Mapinduzi na hii ni kutokana na Ilani yake ya uchaguzi kuweza kutafsirika kwa vitendo hivyo niwaombe msikosee chagueni wagombea wanaotokana na chama hicho" alisema Mbunge Zuena.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI