Mwakilishi wa mauzo wa kampuni ya Oryx wa Mikoa ya Kigoma na Tabora Gibson Rodgers akimkabidhi mmoja wamama wajawazito mtungi wa gesi baada ya kuwapa elimu ya jinsi ya kutumia mitungi hiyo
NA Editha Karlo,Kigoma
KAMPUNI ya oryx energies imekabidhi mitungi ya gesi ya kupikia 300 kwa wanawake wajawazito Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma ikiwa ni kama hatua za kuhakikisha mama mjamzito analea vizuri ujauzito wake ikiwa ni sambamba na kutunza mazingira kwa kutokata miti ovyo.
Akiongea kabla ya kukabidhi mitungi hiyo ya gesi kwa wajawazito katika hospital ya Wilaya ya Buhigwe wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka Taasisi ya Doris Mollel Foundation na Tume ya ushindani ya haki(FCC) Makamu wa Rais Dkt Philipo Mpango aliipongeza kampuni ya oryx kwa kutoa mitungi hiyo,Hiyo inaonyesha jinsi gani wanavyomthamini mama mjamzito na kiumbe chake alichonacho tumboni.
Dkt Mpango alisema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa ikifanya maboresho makubwa katika sekta ya afya,hususani afya ya mama na mtoto ikiwemo afya ya mtoto njiti.
“Niipongeze Taasisi ya Doris Foundation pamoja na taasisi zingine walizoshirikiana kwa mchango wao wa kusaidia jamii ya watoto njiti pamoja na kufanikiwa kuleta vifaa tiba kwaajili ya watoto njiti katika Wilaya ya Buhigwe”alisema Mpango
Awali Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation ameeleza sababu ya kuomba mitungi hiyo ya gesi ya kupikia kwaajili ya wamamawajawazito alisema anatambua changamoto wanazokumbana nazo hivo ni vyema wakaachana na kutumia kuni badala yake watumie majiko ya gesi kwaajili ya usalama wao pamoja na mtoto aliyetumboni.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Oryx Alex Wambi ambaye ni meneja mauzo kanda ya kaskazini alisema kuwa wameamua kutoa mitungi hiyo ya gesi kama zawadi kwa akina mama wajawazito kwasababu wanajua changamoto wanazopita akina mama hao katika kipindi hicho.
“Kipindi mama anakuwa mjamzito huwa anakutana na changamoto nyingi kama asipozidhibiti mapema zinaweza kumletea matatizo na kupelekea kujifungua mtoto ambaye hajatimiza umri(njiti)ndiyo maana tumewapa hawa akina mama haya majiko ya gesi pamoja na elimu ya jinsi ya kuyatumia vizuri”alisema
Naye mmoja wa akina mama wajawazito aliyepata jiko la gesi na mtungi wake aliishukuru kampuni ya oryx kwa kuwapatia majiko hayo pamoja na kuwasadia katika kulinda afya zao na watoto pia itasaidia kutunza mazingira.
“Tunaipongeza serikali na oryx kwa msaada waliotupa wa haya majiko ya gesi,tunaomba wahusika wa waliotupa hii mitungi ya gesi waangalie namna ambayo tutaweza kuipata kwa bei nafuu huku vijijini bei ambayo tutaweza kuzimudu”alisema
Mwisho
0 Comments