NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
CHAMA cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro kimesema kuwa kitawachukulia hatua Watumishi wote wa Umma wenye nia ya kukisababishia chama hicho ajali katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani pamoja na uchaguzi mkuu 2025 kabla dhamira hiyo haijatimia.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Patrick Boisafi wakati wa kikao cha Halmashauri kuu ya CCM mkoa kupokea taarifa utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambapo alisema kuwa wapo baadhi ya Watumishi ambao wanania ya kukisababishia ajali chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.
“Jukumu la kila Mtumishi wa umma ni kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi bila kujali kipato chake lakini wapo baadhi yenu mmekuwa hamtekelezi wajibu wenu na kupelekea kuwachonganisha wananchi na chama chao cha Mapinduzi sasa watu kama hao sisi kama chama kabla yaa kuadhibiwa na wananchi wetu tutawachukulia ninyi hatua mapema” alisema Boisafi.
Alisema kuwa, kazi ya chama cha Mapinduzi ni kuielekeza Serikali ifanye nini ambapo kwa sasa fedha nyingi zimetolewa kwa ajili ya miradi mbalimbali na kuwataka watumishi kusimamia fedha hizo ili thamani yake iweze kuonekana na jukumu la CCM ni kufwatilia fedha hizo.
Aliwataka watumishi hao kutambua kuwa fedha hizo zinazotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani sio siri na kuwataka kujijengea tabia ya kubandika katika mbao za matangazo ili kila mwananchi atambue serikali inafanya nini na imetoa shilingi ngapi ili waweze kufwatilia utekelezaji wake.
“Fedha za miradi zinapokuja na Watendaji mkazitumia kinyume na malengo yaliyokusudiwa mnaenda kukitengenezea ajali chama cha Mapinduzi kwa kutuchonganisha na wananchi sisi kama mkoa hatupo tayari hili litokee tutashughulika na watu hao” alisema Boisafi.
Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka Watumishi wa Umma wanaoona hawawezi kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni kupisha ili waajiriwe watu wengine ambao watafuata utaratibu unaotakiwa katika kuwahudumia wananchi.
Chama hicho pia kilitoa tamko la kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani kwa jinsi anavyolitumikia Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo na kufungua fursa mbalimbali za maendeleo.
Aidha walimpongeza juu uwekezaji wa Bandari ya Dar es salaam ambapo alisema kuwa kuwekezwa kwa bandari hiyo kutafungua fursa ya maendeleo kwa wananchi.
Mwisho..
0 Comments