Header Ads Widget

ASKARI WA WANYAMAPORI AJERUHIWA AKIMUUA SIMBA KIJIJI CHA IRAMBO KILOLO ,RC IRINGA ATOA ZAWADI


Na Matukio Daima Media 

ASKARI  mmoja  wa  wanyamapori amejeruhiwa  usoni na mguuni  wakati  akipambana  kumuua   mmoja kati ya  Simba  aliyekuwa  akitishia maisha  ya  wananchi wa  wilaya ya   Kilolo mkoani  Iringa .


Akizungumza na  Matukio Daima Media katika  uwanja  wa Luganga  wilayani  Kilolo ambako  Simba  aliyeuwawa  alikuwa  ameletwa  Leo asubuhi  kamishina  msaidizi  wa  hifadhi  ya mamlaka ya usimamizi  wa wanyamapori  Tanzania  (TAWA )  Joachim  Makwai  alisema  kuwa  matukio  ya  Simba  yalianza  toka  Juni 13  mwaka  huu  kwa  Simba  kushambulia  mifugo  ya  wananchi .


Alisema  kuwa  kutokana na  matukio hayo  kuendelea  kuwa  tishio askari  wa  TAWA walianza  ufuatiliaji  wa karibu  na kuweka  mitego katika maeneo yote  ambayo  Simba wamepita na kuua  mifugo .


Hata  hivyo  alisema  kuwa  juzi hao  walikuwa  wameua  nguruwe katika  kijiji  cha  Iramba wilaya ya  Kilolo  hivyo  askari  hao  walifanikiwa  kuweka  mitego  katika  eneo  ambalo  Simba  hao  walikuwa  wakilala .


Kuwa kazi  hiyo  ilifanywa na TAWA  ,taasisi ya  utafiti  wa  wanyamapori Tanzania na  madaktari  wa mifugo   ambao  walifanikisha  kumnasa  mmoja kati ya  Simba  hao kwa  mitego na  eneo  ambalo  alikuwa amenasa  lilikuwa ni  vigumu  kumfikia  Simba   huyo na  kumlaza  kwa  kumchoma  Sindano ya  usingizi na  ndipo  walipoamua  kutumia  bunduki  kupambana  nae.


"  Eneo  ambalo  Simba   huyu  alikuwa  amenasa ni sehemu ya  ardhi  oevu  na  ilikuwa vigumu  kumfikia  kumchama  sindano ya  kumlaza  ili  kumkamata akiwa  hai  ndipo  tulipoamua  kutumia  risasi  kwa  kumpiga  na  kutokana  na  kutaka  kujiokoa alimrukia  askari  wetu  mmoja na  kumjeruhi  usoni japo  tayari  alikuwa   hana  nguvu  kutokana na risasi  alizokuwa  amepigwa "  alisema Makwai 



Kuwa askari  huyo aliyejeruhiwa anatambulika kwa  jina la Charlesy  Mafuru  kutoka  TAWA na  baada ya  kujeruhiwa  alikimbizwa   hospitali ya  wilaya ya  Kilolo  ambako  alipatiwa matibabu na  kuruhusiwa .


Makwai  alisema   hadi  sasa  bado  wanaendelea  kufanya  msako kama  kuna  simba mwingine  zaidi  baada ya  Simba  huyo  jike  kuuwawa .



Alisema  simba  hao  waligawanyika katika makundi mawili  kundi  moja alikuwa   eneo la jimbo la  Kalenga kijiji  cha Maboga  ambako inasadikika  alirudi  hifadhini ya Taifa  ya Ruaha  baada ya  matukio  ya  mifugo  kuuwawa  kutotokea  tena  ila  kundi la  pili  ni  hilo la  simba   mmoja alielekea  wilaya ya  Kilolo ambako  tayari  simba  ameuwawa .


Hivyo  aliwataka  wananchi  kuendelea  kuwa  waangalifu  zaidi  hasa nyakati  za  jioni na  usiku  ambao ni muda wa  Simba  kuwinda .


Joseph  Tengelapo  diwani  wa kata ya  Dabaga  alisema  kuwa kabla ya  simba   huyo  kuuwawa    alikuwa  ameua  mbuzi  ,ng'ombe na  Nguruwe  katika  vijiji   vya kata  yake  ili  hawakufanikiwa  kuwapata  simba  hao .




Hata   hivyo  baada ya  matukio  hayo  wananchi  wake wa vijiji  viwili  vya kata  hiyo  waliamua  kujifungia  ndani  muda  wote  bila   kutoka  nje  kutokana na   hofu  kubwa  ya  kuliwa na  simba  hadi  juzi  Simba   huyo  alipofanya  tukio la  kula  nguruwe  eneo la  Shule ya  Msingi  Iramba .



Alisema  kufuatia   tukio   hilo  ndipo askari  hao  wa wanyamapori  waliamua  kuweka  mtego  kijijini hapo na kufanikiwa  kuua  simba   huyo  Leo  asubuhi .


Diwani   huyo  aliishuruku  serikali  na askari  wa  wanyamapori  ambao  wamefanikisha  kuuwawa  kwa  simba   huyo  kwani hofu ya  wananchi  wake  ilikuwa  kubwa  sana  na  hata  shughuli  za  uzalishaji mali  zilisimama  kwenye kata yake kwa  hofu ya  simba .



Kwa  upande wake  askari aliyejeruhiwa na  simba   Joachimu Mafuru  alisema  kuwa   asubuhi  walifanmikiwa  kwenda  eneo  ambalo  walitega  mtego  huo  akiwa na askari  wenzake  watano  na  baada ya  kufika  eneo la  mtego  walisikia mgurumu  wa  simba  ila  hawakujua  yupo  eneo  gani .


Hivyo  wakati  wametawanyika  kumtafuta   Simba   huyo  ndipo  askari  mwenzake  alifanikiwa  kumpiga  risasi  Simba  kifuani na  wakati  Simba  akijaribu  kujitetea ndipo  alipokutana naye  uso  kwa  uso   akitaka  kumrukia  ndipo alipojiokoa kwa  kumfyatulia  risasi  mfululizo   kifuani  hadi  Simba  huyo  alipoanguka  chini .


Alisema  pona  yake  ni  aina ya  bunduki  ya  SMG  aliyokuwa  akiitumia  ndio  iliyomuokoa  kutokana na  kutoa risasi mfululizo  zilizomlenga  simba kifuani .


"  Hili ni  tukio  langu  kubwa la pili  kunusurika  kifo na  wanyama  tukio   jingine  ambalo  sitalisahau  ni lile na kupambana na nyati  aliyejeruhiwa na  nilifanikiwa  kumuua"




Mkuu  wa  mkoa  wa  Iringa  Halima  Dendego  mbali ya  kuwashukuru  askari  hao kwa  ujasiri  walioonesha wa  kufanikisha  kuua  simba   huyo bado  aliungana na  wananchi  kwa  kuwachangia pesa  kiasi  cha  Tsh 500,000 kama ahsante  huku  wananchi  wakichangia shilingi 64000 kuwapongeza  askari  hao .



Mkuu  huyo wa  mkoa  alisema  utaratibu  wa kuwapongeza  zaidi  askari  hao  unafanyika  na  kuwataka  wananchi  kuendelea  kutoa  ushirikiano kwa  askari  hao  na  viongozi  wa  serikali ya  wilaya na  mkoa  kutoa  taarifa   sahihi  za  Simba katika maeneo yao na  kuachana  na  taarifa  za upotoshaji .


Simba hawa Walivamia Makazi ya wananchi wa Jimbo la Kalenga na Kilolo toka Juni 13 mwaka huu na hadi Sasa ni zaidi ya siku 34 na wameuwa Ng'ombe na Nguruwe zaidi ya 56 pamoja na kuku mmoja

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI