NA WILLIUM PAUL, ROMBO.
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amewataka vijana wa Chama hicho ambao ni Chipukizi kuwa wazalendo na nchi kwani wao ni kizazi cha viongozi wa badae watakaolitumikia Taifa.
Mabihya ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kongamano la Chipukizi wilaya ya Rombo ambapo alisema kuwa, nchi inahitaji kuendelea hivyo Chipukizi wanawajibu wa kupigana na maadui Ujinga, Umaskini na Maradhi.
"Mnapaswa kutambua mnaishi katika nchi ya Tanzania hivyo mnawajibu wa kuendelea kulinda na kutunza Tunu za Taifa pamoja na kuilinda na kuitetea nchi na kuwa wazalendo" alisema Mabihya.
Aidha Katibu huyo aliwataka vijana hao kushika Elimu na kuwaonya kutokuwa watoro wa shule ili kuweza kitimiza ndoto zao za badae pamoja na kuwa watii kwa Serikali, Wazazi na watu wengine.
Katika hatua nyingine Mabihya aliwataka kuendelea kufichua vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa katika jamii ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Niwaombe muendelee kukipenda chama cha Mapinduzi kwani ndicho chama kinacholinda Tunu za Taifa pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo na kuwajali" alisema Mabihya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chipukizi wilaya ya Rombo, Ivon Primi alisema kuwa, Chipukizi wilaya ya Rombo wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa sare na kumuomba Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro kuwasaidia kupata sare.
Ivon alisema kuwa, vijana hao wanania ya dhati ya kukipigania chama na kulinda Taifa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kuahidi kuendelea kulinda muungano.
Mwisho..
0 Comments