NA WILLIUM PAUL, SAME.
WATU wawili wamefariki Dunia baada ya gari walilokuwa wakitumia kusafiria kugongana uso kwa uso na basi la abiria la kampuni ya Kilimanjaro Express maeneo ya Majengo kata ya Hedaru wilaya Same mkoani Kilimanjaro.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema kuwa tukio hilo limetokea Juni 23 mwaka huu majira ya saa kumi na mbili asubuhi.
Kamanda Maigwa alisema kuwa, gari mali ya kampuni ya Kilimanjaro Express lenye namba za usajili T. 983 AWY likitokea Arusha kuelekea Dar es salaam liligongana na gari dogo aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 99 CPS lililokuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Moshi na kusababisha vifo vya watu wawili waliokuwa katika gari dogo.
Aliwataja waliofariki katika ajali hiyo, Kamanda Maigwa alisema ni dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo dogo, Martin Mhagama (45), Mrakibu wa Jeshi la Uhamiaji Kurasini jijini Dar es salaam, pamoja na abiria wake Rehema Sekhao (40) mkazi wa jijini Arusha.
Kamanda Maigwa alisema kuwa, kwa sasa wanamshikilia Dereva wa gari la Kilimanjaro Express kwa mahojiano zaidi huku miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Same.
Mwisho.
0 Comments