Na Amon Mtega_Songea.
TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Muunganisho wa Ujasiriamali Mijini na Vijijini (MUMIVI )inayojishughulisha na upandaji pamoja na utunzaji miti ngazi ya jamii imefanya mafunzo ya siku mbili kwa washiriki zaidi ya 171 kutoka Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma ili wakasimamie kikamilifu juu ya utunzaji wa mazingira kwa jamii.
Akizungumza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Koyigila Kazuzi amesema kuwa Taasisi hiyo imefanya mafunzo hayo kwa wawakilishi yaani mabalozi wasimamizi wa mazingira ngazi ya kata pamoja na baadhi ya walimu wa shule za msingi kwa kutumia mfumo shirikishi wa O& OD Tamisemi Taifa baada ya kutambua kuwa kumekuwepo na uharibifu wa mazingira ambayo yamekuwa yakiadhiri jamii na kupelekea mabadiliko ya tabia Nchi.
Kazuzi amesema kuwa kama jamii itazingatia utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti na kutunza vyanzo vya maji , mazingira hayo yatazidi kuboreka na kuvifanya vizazi vijavyo kunufaika na uhifadhi huo.
Kwa upande wake mtaalam wa O & OD toka Tamisemi Silas Samaluku wakati akitoa elimu kwa wawakilishi hao amesema kuwa bila uwepo wa utunzaji wa mazingira hakuna kituchochote kitakachoweza kufanyika kwa kuwa kila kitu kinategemea mazingira .
Samaluku amefafanua kuwa kumekuwepo na baadhi ya wanajamii kuharibu mazingira ikiwemo kuwapoteza wanyama kwa madai kwamba wanyama siyo sehemu ya mazingira jambo ambolo halikubaliki kwa kuwa wanyama hao ni sehemu ya utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo mtaalam huyo amewaambia washiriki hao kuwa wakatoe elimu kwa jamii kuwa wanawajibu wa kila mwanajamii kutunza mazingira bila kutegemea Serikali iwakumbushe .
Naye afisa misitu Wilaya ya Songea Zakayo Kaunda amesema bado kunatatizo la uharibifu wa mazingira hivyo elimu iliyotolewa kwa wawakilishi hao itaenda kukabiliana na tatizo hilo.
Pia Afisa Elimu maalum ambaye ni mdau wa miti katika Halmashauri ya Songea Vijijini Sothery Nchimbi amesema kuwa baadhi ya walimu wa shule za msingi wameshilikishwa kwenye mafunzo hayo ili waweze kwenda kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa utunzaji wa mazingira.
Naye mmoja wa waliyopatiwa mafunzo hayo Irene Mhagama amesema kuwa mafunzo hayo wataenda kuyafanyia kazi kwa kutoa elimu kwa jamii ili iachane na uharibifu wa mazingira kwa kutumia mfumo shirikishi .
0 Comments