Header Ads Widget

SERIKALI KUFIKISHA HUDUMA YA GESI ASILIA VIJIJI VINAVYOZUNGUKA MLIMA KILIMANJARO

 


NA WILLIUM PAUL.

KATIKA kuhakikisha wananchi wanaoishi kuzunguka mlima Kilimanjaro hawaaridu mazingira kwa kukata miti ili kupata kuni Serikali inampango wa kufikisha gesi asilimia katika maeneo hayo.


Hayo yamekuja baada ya Mbunge wa jimbo la Moshi vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi kuuliza swali Bungeni je kuna mpango gani wa kupeleka nishati ya gesi asilia katika vijiji vinavyozunguka mlima Kilimanjaro ili kupunguza matumizi ya kuni.  


Mbunge huyo pia katika maswali yake mawili ya nyongeza alihoji je Wizara ina mikakati gani kuwekeza kwenye Nishati endelevu kama ile ya kupata gesi ya kupikia na kuwasha taa kutoka kwenye kinyesi cha wanyama kama njia mojawapo ya kupunguza matumizi ya kuni. 


"Je Serikali haioni umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya majiko ya mkaa banifu kama vile mkaa tofali utokanao na pumba za mpunga na masalia mengine ya mimea ili kuepukana na kukata miti" alihoji Prof. Ndakidemi.


Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nishati,  Stephen Lujwahuka Byabato alisema kuwa, Gesi asilia inaweza kusafirisha kwa njia ya mabomba au kwa njia ya mitungi au tenki inayobebwa na malori, treni au meli ambapo Gesi asilia inakuwa katika hali ya gesi iliyoganda au kimiminika.


Naibu Waziri Byabato alisema kuwa, hadi sasa gesi asilia inachimbwa Mtwara na hivyo maeneo yaliyounganishwa na kuweza kutumia nishati ya gesi asilia ni yale yaliyopitiwa na miundombinu ya mabomba ya kusafirisha gesi ambayo ni mkoa wa Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es salaam.


"Mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kwenda Mombasa nchini Kenya kupitia mkoa wa Tanga ni moja ya miradi inayotoa fursa ya kuunganisha mikoa ya Kaskazini na gesi asilia ikiwamo na mkoa wa Kilimanjaro kwa kuweka toleo katika eneo la Segera mkoani Tanga" alisema Naibu Waziri Byabato.


Na kuongeza "mradi huu wa bomba bado unafanyiwa kazi serikalini utakapokamilika gesi asilia itaweza kufikishwa mkoani Kilimanjaro ikiwemo vijiji vinavyozunguka mlima Kilimanjaro na katika maeneo mengine mkoani humo na mikoa ya jirani".


Alisema kuwa, tangu mwaka jana Rais Dkt Samia Suluhu Hasani alizindua mjadala wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia na ni azma ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati wamekuwa wakijikimu kuelekea kwenye nishati safi ya kupikia.


Alisema kuwa katika eneo hilo wanahamasisha utumiaji wa gesi ya mitungi, lakini gesi asilia na maeneo mengine kutumia kinyesi cha wanyama na mikaa ya kutengeneza.


Wizara ya Nishati kupitia Rea imekuwa ikiwezesha na kugharamia wale wagunduzi na watengenezaji wa majiko banifu na mikaa ya asili na wataendelea kuwasimamia wananchi na kuwawezesha na kuwapa pesa za mitaji ili kupata vitendea kazi na kuzalisha gesi ya kupikia na kuwasha taa.


"Nikushukuru Prof. Patrick Ndakidemi kwa ufwatiliaji wa eneo hili ambalo ni jipya ambapo Serikali imetilia mkazo kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia nishati safi hasa ya kupikia" alisema Naibu Waziri Byabato.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI