Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Rabani Thomas
Na Amon Mtega, Mbinga
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Rabani Thomas amemtaka mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbinga mji Amina Seif pamoja na wakuu wake wa idara kutumia zaidi wakaguzi wa hesabu wa ndani ili kuepuka kupata hati chafu au zenye mashaka pindi mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) anapopitia kukagua mahesabu hayo.
Wito huo ameutoa wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mbinga mji ambalo limekuwa rasmi kujadili hoja za mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali ili ziweze kujibiwa ambapo Halmashauri hiyo imepata hati ya mashaka.
Kanali Rabani akizungumza kwenye kikao hicho amesema kuwa hati nyingine za mashaka au chafu hupatikana kutokana na kutokuwatumia wakaguzi wa ndani jambo ambalo halitakiwi.
Aidha mkuu huyo amezitaka hoja hizo zilizoipelekea Halmashauri hiyo kapatiwa hati ya mashaka zijibiwe mapema ili kuifanya Halmashauri hiyo izidi kusongambele kwa maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho ameipongeza Halmashauri hiyo kuwa imekuwa ikipata hati safi mfululizo kwa muda wa miaka mitano tofauti na mwaka huu ambapo imepata hati ya mashaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbinga mji Kelvin Mapunda wakati akihitimisha kikao hicho amesema kuwa Halmashauri hiyo imejipanga vema katika kukabiliana na hati ya mashaka ili zisiwepo huku akimuahidi mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Rabani Thomas kuwa maagizo yote alioyatoa yatafanyiwa kazi kwa wakati.
Mwenyekiti Mapunda pia ametumia nafasi hiyo ya kumtambulisha mkurugenzi mpya wa Halmashauri hiyo Amina Seif ambaye ni mara yake ya kwanza kuitumikia nafasi hiyo.
0 Comments