Na,Jusline Marco;Arusha
Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati Dkt.Solomon Jacob Masangwa amelitaka kanisa na jamii kuzidi kukemea na kupinga vitendo vya ushoga huki akiitaka jamii kuwekeza elimu sahihi kwa watoto wao.
Askofu Dkt.Masangwa ameyasema hayo katika ibada ya Maadhimisho ya Yubile ya Miaka 50 ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati yaliyofanyika kwenye Usharika wa Iliboru ambapo amesema ni vyema watoto wakafundishwa katika njia iliyo njema.
Amesema kuwa katika kukemea na kupinga vitendo hivyo viovu ni vyema elimu sahihi ikawekezwa kwa vijana wangali wakiwa wadogo ili waweze kutambua kuwa vitendo hivyo ni vibaya na nichukizo kwa Mwenyenzi Mungu hali ambayo itasaidia kutoyasikiliza mafundisho potofu ya nje .
Baba Askofu Dkt.Masangwa amewataka watoto katika Dayosisi hiyo kumshika Mungu huku wakiwatii wazazi,walezi,waalimu wao na kuwasikiliza na kuzingatia mafundisho wanayopatiwa ambayo yatawasaidia kuendelea kuwa vichwa na siyo mkia.
Aidha amewataka wakristo kutokuwa watu wa kutoa sababu na udhuru wa utekelezaji wa wajibu wao bali wawe watu wenye mtazamo chanya katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ambapo amesema Dayosisi ya kaskazini kati ina mipango mikakati katika kipindi cha miaka 25 ijayo.
"Mungu anapotupa fursa ya kuingia mwaka wa 51 na nafasi za utumishi tusiwe watu wa kutoa sababu na udhuru kushindwa kutekeleza wajibu wetu maana huyu Mungu ambaye tunamtaja anaweza mambo yote kwanini tushindwe jambo lolote katika maisha ya kanisa?"alisisitiza Baba Askofu Dkt.Solomon Masangwa
Dkt.Masangwa amesema kuwa katika Dayosisi ya Kaskazini Kati wanayo mipango mikakati ya miaka 5 na hakuna sababu ya kushindwa kutekeleza mipango mikakati hiyo ambapo amesema katika miaka 25 ijayo pasiwepo na kiongozi atakayetoa udhuru na kuiharibu kazi ya Bwana kuanzia ngazi ya familia,jumuiya ,mtaa,usharika ,jimbo,dayosisi,kanisa na hata taifa.
"Udhuru au sababu za kushindwa kutekeleza wajibu wetu watu wakiacha kutoa sababu na kuanza kutatua matatizo yanayowakabili katika maeneo yao kwa utaratibu inakuwa ni afya kwa jamii na taifa kwa ujumla."alisema Dkt.Masangwa
Ameongeza kuwa waumini na viongozi wa dini hususani Kanisa la KKKT wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanafundisha elimu ya kikristo kutoka familia kuelekea katika shule za msingi na sekondari pamoja na elimu za juu.
Awali akisoma histori ya Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo, Robert Martin Kitundu amesema Dayosisi ya Kaskazini Kati inatoa huduma ya injili ikimhudumia mwabadamu kiroho,kimwili na kiakili katika mikoa ya Arusha na Manyara ikiwa na majimbo 7 ambayo ni Arusha Mashariki,Arusha Magharibi,Babati,Maasai Kaskazini,Maasai Kati,Maasai Kusini Kati na Jimbo la Kusini.
Ameongeza kuwa Dayosisi hiyo ilianzishwa mnamo mwaka 1973 ikijulikana kwa jina la Sinodi Mkoani Arusha ikiwa na washirika elfu 30 na sharika 20 pamoja na mitaa 110 ambapo mwaka 1986 Sinodi ilibadili jina na kuwa Dayosisi Mkoa wa Arusha na mnamo mwaka 2010 Dayosisi Mkoa wa Arusha ilibadili jina na kuwa Dayosisi ya Kaskazini Kati.
Vilevile amesema kuwa Dayosisi kwa sasa ina sharika 123 mitaa 920 na washirika laki 308000 pia ina hospitali 3,zahanati 7,kituo cha afya 1,chuo 1 cha Nursing ,hotel 1 ya kitalii,chuo cha theolojia Oldonyosambu,shule za msingi 3,shule za sekondari 6,chuo cha ufundi 1 na chuo cha kati cha biashara 1.
Katika hatua nyingine Mkuu wa jimbo mstaafu mch.Joel Ole Nangole akisoma nakala fupi ya Yubilee hiyo amesema katika kuheshimu mpango wa Mungu wa uumbaji unaosimamiwa na maandiko matakatifu ,dayosisi ya kasazini kati inapinga na kukataa kwa nguvu zote ndoa za jinsia moja ulawiti,ushoga na usagaji ambao ni kinyume na tamaduni za kiafrika na ni chukizo kubwa mbele za mungu.
Ameongeza kuwa Kauli Mbiu ya maadhimisho hayo imejengwa katika maandiko matakatifu ambapo amesema Yubilee hiyo inaandamana na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika na mwaka wa uhuru na kufunguliwa ikiwa ni pamoja na kupanda miti laki 3 katika maeneo ambayo Dayosisi imeenea kihuduma ili kuweza kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yameweka msisitizo katika kuimarisha Uinjilisti na huduma ya Udiakonia kuwa kuwafikia wahitaji na kuwainua katika dhiki zao ili waweze kujitegemea na kuwasaidia wengine,kuimarisha afya kwa jamii ambapo pia suala zima la elimu limeguswa katika maadhimisho hayo katika Dayosisi hiyo.
0 Comments