Header Ads Widget

UKARABATI NA UPANUZI KATIKA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA WAANZA RASMI, WANANCHI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Serikali imesema  zaidi ya Shilingi Bilioni 49 zitatumika kukarabati na kupanua  uwanja wa ndege wa Shinyanga,kwa ufadhili wa Benki ya uwekezaji ya Ulaya (EIB).

Katika taarifa yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, TANROADS  na wadau wengine wa usafiri wa anga, Meneja miradi viwanja vya ndege TANROADS Nchini, Mhandisi Neema Joseph amesema mradi huo umeanza Aprili Mwaka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka 2024.

Meneja huyo amefafanua hatua mbalimbali zilizofikiwa ikiwemo ukarabati wa Barabara ya kutua na kurukia ndege, ununuzi na usimikaji wa mitambo ya usalama pamoja na ujenzi wa jengo la abiria.

“Kiwanja cha ndege Shinyanga ni miongoni mwa viwanja vya ndege muhimu Nchini, kiwanja hiki kinatarajiwa kuharakisha usafiri kwa wananchi pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi hususani katika sekta za madini na kilimo”.

“Kazi zinazofanyika ni ukarabati wa barabara ya kutua na kurukia ndege (Runway) kwa kiwango cha lami, ukarabati wa barabara ya kiungio na maegesho ya ndege kwa kiwango cha lami, ujenzi wa jengo la abiria ( pamoja na ATC) na huduma za hali ya hewa lakini pia ujenzi wa barabara ya kuingia uwanjani”.

“Kazi zingine pia ni ujenzi wa maegesho ya magari, ujenzi wa uzio wa usalama, ununuzi na usimikaji wa taa za kuongezea ndege (AGL), ununuzi na usimikaji wa mitambo ya usalama (DVOR\DME) pamoja na ujenzi wa kituo cha umeme (Enegry centre) tunatarajia wadau wote mtatupa ushirikiano katika kufikia lengo hili”.amesema Mhandisi Neema Joseph

Akizungumza katika mkutano huo uliohusisha wadau wa usafiri wa anga na TANROADS, mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Johari Samizi ambaye alikuwa mgeni rasmi ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Shinyanga na maeneo mengine ya Mkoa  kutambua na kuzichangamkia fursa zitakazojitokeza katika mradi huo.

DC Samizi amewakumbusha pia wakala wa barabara TANROADS Mkoa wa Shinyanga kusimamia ipasanyo hatua zinazoendelea za ukarabati na upanuzi katika uwanja huo wa ndege ili uweze kukamilika kwa wakati na kwa  kiwango kinachotakiwa.

“Nitoe rai yangu kwa TANROADS hili jukumu mnatakiwa mlisimamie linavyotakikana thamani ya fedha ambayo inakwenda kuwekwa hapa ionekane siku ambayo mradi huu unakwenda kukamilika na kukabidhiwa”.amesema DC Samizi

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga mhandisi Mibara Ndirimbi ameahidi kusimamia mradi huo kikamilifu  ili uweze kukamilika  kwa wakati  na kiwango chenye ubora ambapo amewaomba wananchi kushirikiana katika ulinzi wa mali zitakazotumika kwenye mradi huo.

Baadhi ya wadau  waliohudhuria hafla hiyo wameipongeza serikali kwa hatua hiyo na kwamba wameahidi kuendelea kushirikiana katika hatua mbalimbali za mradi huo ili kuleta matokeo chanya Mkoa wa Shinyanga.

Wakala wa barabara TANROADS Mkoa wa Shinyanga leo Mei 30, 2023 wamekutana na wadau mbalimbali wa usafiri wa anga hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, viongozi wa chama na viongozi wa dini kwa lengo la kujadili hatua mbalimbali katika ukarabati na utanuzi uwanja wa ndege Mkoa wa Shinyanga.



Mkutano wa wadau wa usafiri wa anga na TANROADS ukiendelea katika eneo la uwanja wa ndege wa Mkoani Shinyanga leo Mei 30,2023

Mdau wa usafiri wa anga, meneja usalama mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania Bwana Clemence Jingu Mbaruck  akimwakilisha mkurugenzi wa TAA katika mkutano wa Wadau wa usafiri wa anga na TANROADS kwenye  uwanja wa Ndege wa Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS