KATIKA kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, Benki ya NMB na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU), ambayo yamepongezwa na SMZ, iliyokiri kuwa taasisi hiyo kinara ya fedha nchini ni mbia bora na sahihi katika kuhimili vita ya ushindani kwenye Sekta ya Uwekezaji Afrika.
Makubaliano hayo yamesainiwa Zanzibar Mei 9, yakilenga kuendeleza ushirikiano katika kutengeneza mifumo ya kufuatilia taarifa na kuwadumia wawekezaji visiwani hapa, sanjari na kutangaza vivutio vya uwekezaji nchini, pamoja na NMB kutoa suluhishi za kifedha na ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali kwa wawekezaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Mudrik Ramadhani Soraga, alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, akishuhudia utiaji saini huo uliofanywa na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna na Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Sharif Sharif, mbele ya Dkt. Khatibu Mwadini, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Soraga aliishukuru na kuipongeza NMB kwa aina ya ushirikiano inaotoa kwa Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar inayoongozwa na Rais, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikiwemo udau katika kukuza Uchumi wa Buluu na sasa kuipa nguvu za kuhimili ushindani katika Uwekezaji, pamoja na kusapoti mabadiliko ya kiutendaji kwa njia ya kidigitali ya Serikali na taasisi zake.
"Aina ya ushirikiano wa NMB kwa Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar ni wa kuigwa, ikiunga mkono kila jitihada za kutoa huduma bora na kukuza ufanisi katika kuvutia wawekezaji na nikiri kwamba isingekuwa rahisi kwa SMZ na taasisi zake kupata mbia bora na sahihi zaidi ya NMB.
"Usipofanya ukuzaji huwezi kushindana na usiposhindana huwezi kukuza uwekezaji. NMB imetupa nguvu hiyo, ikiwezesha watendaji wa taasisi Serikali kwenda nje ya nchi kujifunza namna ya kukuza ufanisi katika uwekezaji," alisema Waziri Soraga.
Awali, Zaipuna aliishukuru ZIPA na SMZ kwa kuikaribisha NMB kuwa mshirika wa karibu katika safari ya kuiletea Zanzibar maendeleo chanya ya kiuchumi na kijamii na kusisitiza ya kwamba benki yake inatambua na kuheshimu nia ya dhati ya Serikali kupitia ZIPA, ya kuishirikisha taasisi yake katika utekelezaji wa mipango ya kuwahudumia wawekezaji kwa ufanisi zaidi.
Alifafanua ya kuwa, Machi mwaka huu, SMZ kupitia ZIPA, ilizindua muongozo wa uwekezaji Zanzibar na mfumo wa kielektroniki wa kuhudumia wawekezaji, ambapo kupitia mfumo huo, Wawekezaji waliweza kujisajili, kufanya maombi ya cheti cha uwekezaji, mpaka kupata cheti cha uthibitisho wa uwekezaji wao.
0 Comments