NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MWILI wa aliyekuwa Diwani wa kata ya Old Moshi magharibi wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Menyasumba Macha aliyefariki Mei 15 mwaka huu kwa ajali ya gari umezikwa leo kijijini kwao Mande.
Zoezi la kutoa heshima za mwisho kwa marehemu Diwani huyo zilianza katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Moshi (KDC) ambapo Madiwani, wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri hiyo walipata nafasi za kutoa heshima za mwisho.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Moris Makoi alisema kuwa Halmashauri imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo.
"Siku ya Mei 12 mwaka huu tulikuwa na kikao cha maandalizi ya baraza la Madiwani (pre-baraza) na marehemu alishiriki kikao hicho ambapo alitoa hoja za muhimu kwa maslahi mapana ya wananchi wake wa kata ya Old Moshi magharibi" alisema Makoi.
Makoi alisema kuwa, mnamo Mei 15 mwaka huu walipokea kwa mshituko kifo chake kwani siku hiyo ndio ilikuwa siku ya kikao cha baraza la Madiwani na kupelekea kuahirisha kikao hicho.
Alisema kuwa, sifa kubwa aliyokuwa nayo marehemu ni kupambana kwa hoja katika kuhakikisha anatetea maslahi ya wananchi wake na wao kama Madiwani wataendelea kuyaishi yale yote mema yaliyokuwa yakifanywa na Diwani huyo enzi za uhai wake.
"Kila mmoja anashindwa kuamini kilichotokea lakini wakati wa bwana ukifika hauzuiliki hivyo wakati wa Macha umefika hatuwezi kuzuia tunachofanya ni kumuomba" alisema Makoi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa, Macha alikuwa ni kiongozi yapo mazuri alikuwa akiyafanya kwa ajili ya wananchi wa kata ya Old Moshi magharibi na mimi nimuombe msamaha kwa yale aliyoshindwa kuyakamilisha wakati wa uongozi wake.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi vijijini, Ramadhan Mahanyu alisema kuwa, chama kimepoteza mwakilishi mzuri mpiganaji na mtetezi wa wananchi na Halmashauri ya Moshi.
Mahanyu alisema kuwa, marehemu alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kata yake ya Old Moshi magharibi inapata maendeleo makubwa hivyo CCM inatoa pole kwa familia ya Macha na wananchi wa kata hiyo kwa kuondokewa na kiongozi shupavu.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kisare Makori alisema kuwa kifo cha mwanadamu ni fumbo kubwa lililowekwa na Mwenyezi Mungu na kuwatia moyo wanafamilia kuwa na ujasiri katika kipindi hiki kigumu.
Makori alisema kuwa, Macha ametangulia na kila mmoja atapita katika njia hiyo hivyo wanachopaswa kufanya ni kumuomba pumziko la amani.
Aidha amewataka wanafamilia na Madiwani wenzake kuyaishi yale yote mazuri ambayo alikuwa akiyafanya Macha enzi za uhai wake.
Marehemu Menyasumba Macha alizaliwa mnamo Mei 16 mwaka 1963 na kufariki Mei 15 mwaka huu ambapo ameacha mke na watoto wanne na mjukuu mmoja.
Mwisho..
0 Comments