NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
WANANCHI wa vitongoji cha Njia panda Mashariki, Faru na Darajani katika mji mdogo wa Himo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wanakabiliowa na tatizo la ukosefu wa mawasiliano ya barabara ya kuingia na kutoka katika kitongoji hicho baada ya barabara ya Elimo waliyokuwa wakiitumia kusombwa na maji.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa uchungu mkubwa wananchi hao Yolanda Kimario alisema kuwa, kipindi hiki cha mvua wamekuwa wakilazimika kuwazuia watoto kwenda shule kutokana na kuhofia maji ya mvua yanayotiririka kwa wingi katika makorongo yaliyopo kitongoji hapo.
Alisema kuwa, kwa sasa usalama wa watoto ni mdogo wanapoenda shule hali ambayo imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wazazi kuhakikisha wanawapeleka na kuwarudisha watoto nyumbani kutokana na barabara zilizokuwa zikiingia katika vitongoji hivyo kusombwa na maji.
Naye Yetonsia Kiring’a alisema kuwa, kwa sasa wakinamama wajawazito wamelazika kujifungulia nyumbani kutokana na magari kushindwa kufika kuwachukua na kuwapeleka haspitali hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha ya mtoto pamoja na mama.
“ Wapo ndugu zetu wagonjwa tumeshindwa kuwafikisha hospitali kutona na kukosa barabara na wakati mwingine inapobidi tumekuwa tukiwabeba mgongoni na kwenye machela kuwatoa barabara kuu ili waweze kupata huduma ya usafiri tunaiomba sana serikali ituangalie kwa jicho la kipekee” alisema Yetonsia.
Naye Jemsi Maleko alisema kuwa mkazi wa Kitongoji cha Njia panda mashariki alisema kuwa, kwa sasa wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na barabara kuu ya kuingia na kutoka katika kitongoji hicho kuwa mbaya na magari kushindwa kupita hali inayowalazimu kulaza magari yao katika vituo vya mafuta Njia panda na Himo.
Maleko alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kufanya juhudi za haraka kurejesha mawasiliano ya barabara ya Elimo ili kuwaondoa wananchi wa Vitongoji vya Faru, Njia panda mashariki na Darajani ambao kwa sasa ni sawa na wapo katika kisiwa.
Akielezia kuhusu kero hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Mji Mdogo wa Himo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Darajani, Richard Njau alise kuwa wananchi wanahaki ya kulalamika kutoka na kuitegemea barabara ya Elimu kuingia na kutoka ambapo kwa sasa haipitiki baada ya kusombwa na maji.
Njau alisema kuwa, kutokana na uharibufu uliotokana na mvua upelekea watoto kushindwa kwenda shule na hata wakinamama wajawazito kushindwa kwenda kliniki na hata wakati mwingine hospitali kujifungua pindi wanapofikia.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuwaomba Wakala wa Barabara vijijini (TARURA), kufika haraka katika vitongoji hivyo na kutafuta njia ya haraka ya kuwanusuru wananchi hao ambapo mpaka sasa hawajui hatima yao hasa kipindi hiki cha mvua.
Naye Mwenyekiti wa shina namba mbili kitongoji cha Njia panda mashariki, Faustin Abel alisema kuwa ameshachukua hatua za haraka za kumshirikisha Diwani wa kata ya Njia panda, Loveness Mfinanga kuhusu kuharibika kwa barabara hiyo ambayo Diwani huyo alimuahidi kulifikisha tatizo hilo tarura.
“Tangu kuharibika kwa barabara hii kumepelekea watoto kutokwenda shule lakini pia baadhi ya watumishi wa umma kushindwa kwenda katika vituo vyao vya kazi kwani maji yanayopita katika barabara hii ya Elimo ni mengi nan i hatari kwa maisha yao” alisema Abel.
Mwisho..
0 Comments