NA HADIJA OMARY, MATUKIO DAIMAAPP LINDI
WAKURUGENZI wa Halmashauri Nchini wametakiwa kuendelea kusimamia afua mbalimbali za mfumo wa ugavi wa bidhaa za Afya ikiwa pamoja na kufanya ufuatiliaji bidhaa (medicine audit) sambamba na kupeleka taarifa tamisemi kama mwongozo unavyotaka.
Wito huo umetolewa na Naibu katibu Mkuu TAMISEMI -Afya Dkt. Wilson Mahera wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa kielekroniki wa mshitiri kwa wataalamu wa Afya Mkoani Lindi yaliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa hospital ya Rufaa Mkoa wa Lindi Sokoine .
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Dkt. Wilison Mahera alisema Mfumo huo wa mshitiri utakwenda kukomesha mianya ya Rushwa sambamba na kufanya kuwa na matumizi bora ya dawa kwa maslahi ya umma pamoja na kupunguza changamoto zinazotokana na usimamizi wa bidhaa hizo.
Alisema mfumo huo wa mshitiri kielekroniki umewekwa mahususi na Serikali kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa Dawa katika vituo vya kutolea huduma pale ambapo MSD dawa hizo zitakapokosekana kwa wakati huo
“mfumo huo ni wa kielekroniki ambao serikali umeuweka kwa ajili ya pale ambapo dawa zitakuwa zimekosekana MSD basi washitiri wanakuwa wameshabainishwa katika kila Mkoa ili dawa ziweze kupatikana kwa uharaka zaidi na inapotokea kama unachangamoto ya dawa katika eneo lako inajulikana unakwenda kuchukua dawa kwa mshitiri aina gani hivyo gharama za dawa zinakuwa ni saw ana zile za MSD ”
Hata hivyo Dkt. Wilson Mahera pia aliwataka wakurugenzi katika halmashauri zao kupitia mapato yao ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa kopyuta zitakazofungwa katika vituo vya Afya zitakazosaidia kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
Kwa upande wake mganga mkuu wa Mkoa wa Lindi Kheri kagya alisema mfumo huo licha ya kuziba mianya ya Rushwa katika uagizaji wa dawa na kuwapata wazabuni pia utasaidia upatikanaji wa dawa kwa wakati pale changamoto inapotokea tofauti na hapo awali.
Hata hivyo alibainisha kuwa hali ya upatikanaji wa Dawa ndani ya Mkoa huo imeendelea kuimarika kutoka asilimia 88.6 kwa mwaka 2022 mpaka kufikia asilimia 91. 5 kwa sasa
0 Comments