Na Fadhili Abdallah,Kigoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoa Kigoma kimetoa maelekezo kwa ofisi ya Mkuu wa wilaya Uvinza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuwakamata na kuwafungulia mashitaka viongozi wa vijiji ambao wameuza maeneo ya vijiji vyao kinyume cha sheria.
Katibu wa CCM mkoa Kigoma,Mobutu Malima ametoa maelekezo hayo akizungumza kwenye mkutano na viongozi wa vijiji, Wenyeviti na Makatibu wa kata za wilaya ya Uvinza na kubainisha kuwa matendo yaliyofanywa na viongozi hao wa vijiji hayakubaliki.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wenyeviti wa vijiji 45 kati ya vijiji 61 vilivyopo kwenye wilaya hiyo Malima alitoa maelekezo kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa wenyeviti wa vijiji vitano ambao wamekuwa vinara wa uuzwaji wa maeneo kwenye vijiji vyao kwa kukiuka sheria.
Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni pamoja na Mgambazi, Chakuru, Rukoma, Lufubu na Malagarasi ambapo wenyeviti hao wanadaiwa kuuza hadi Heka 1000 kwa mtu mmoja wakati sheria haiwapi mamlaka hayo.
Akizungumza katika kikao cha ndani kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ya Uvinza Mwenyekiti wa CCM wa wilaya hiyo, Emanuel Kalayenga alisema kuwa baada ya uchaguzi wa chama amefanya ziara na kamati ya siasa ya wilaya nakushuhudia changamoto kubwa ya matumizi mbaya ya madaraka ya viongozi wa vijiji wengi wakilalamikiwa kwa ubabe, jeuri na kujichukulia sheria bila kufuata taratibu.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema kuwa uuzwaji wa maeneo ya ardhi za vijiji imekuwa changamoto kubwa ambapo viongozi hao wameuza maeneo kwa mtu mmoja kinyume na sheria za ardhi na mamlaka na madaraka yao huku jambo hilo likifanywa na watu wachache bila kuhusisha serikali za vijiji wala kupata ridhaa za wananchi.
Katika Mkutano huo Katibu wa CCM kata ya Mgambazi, Salim Mohamd alisema kuwa kwa sasa maeneo yote ya vijiji vya kata hiyo yana hali mbaya hasa kijiji cha Mgambazi ambapo Mwenyekiti wa kijiji ameuza sehemu kubwa ya ardhi ya kijiji hicho bila kufuata utaratibu.
Mohamed alisema kuwa maeneo hayo yameuzwa kwa wafugaji kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambao wameingiza makundi makubwa ya ng’ombe lakini wakivuruga mipango ya matumizi bora ya vijiji iliyowekuwa imewekwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Uvinza, Masumbuko Kechegwa alisema kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ikiwemo kusimamishwa kwa wenyeviti wa vijiji ikiwemo kijiji cha Lufubu ambapo Mwenyekiti wake anatuhumiwa kuuza eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta 1000.









0 Comments