Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Jumuiya ya wazazi ya CCM mkoa (UWT) imetoa kauli na kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia unaofanywa majumbani na mapenzi ya jinsia moja na kuwataka watanzania kutokubali kuiga mambo ambayo ni kinyume na utamaduni wetu.
Kauli hiyo imetolewa na wajumbe wa baraza kuu la mkoa la UWT katika kongamano la wanawake lililofanyika mjini Kigoma ikiwa ni kuelekea kilele cha siku ya wanawake inayotarajiwa kufanyika Machi 8,2023 na mkoa Kigoma kimkoa itafanyika katika kijiji cha Mahembe halmashauri ya wilaya ya Kigoma.
Akitangaza maazimio hayo mbele ya wajumbe hao Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kigoma, Agripina Buyogera alisema kuwa jumuiya hiyo haikubaliani na vitendo vya ukatili wa kijinsia unaofanywa majumbani kwani umekuwa na athari kubwa kimwili na kiakili kwa watu mbalimbali lakini akabainisha kuwa wanawake na watoto ndiyo waathirika wakubwa wa vitendo hivyo.
Sambamba na hilo alisema kuwa kwa nguvu moja wanalaani mapenzi ya jinsia moja ambayo yanaonekana kushika kasi nchini na kusema kuwa lazima waungane ni vitabu vya dini ambavyo vinapinga vitendo hivyo ambapo wameiomba serikali kuchukua hatua kali zinazoweza kukomesha vitendo hivyo.
Mwenyekiti huyo wa UWT mkoa Kigoma amewataka wanawake hao kwenda kujipanga na kugombea nafasi mbalimbali kwenye meneo yao wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Awali akitoa mada katika kongamano hilo mmoja wa maafisa wa dawati la jinsia la jeshi la polisi mkoa Kigoma, Pilly Ringo alisema jamii kushindwa kutoa taarifa za matendo ya ukatili yaliyofanyika au kuchelewa kutoa taarifa hizo kumesababisha kupoteza ushahidi unaotakiwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wanaotenda vitendo hivyo.
Alisema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili, unyanyasaji kijinsia lakini wakati mwingine taarifa kwa wahanga hazitolewi na kwamba hali hiyo inaweza kuchochea kuendelea kwa vitendo hivyo kwani alibainisha kuwa kutolewa taarifa kunawezesha mamlaka kufuatilia na watuhumiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali.
Mjumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM, Joyce Mang’o ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hiloaliwataka wanawake nchini kuendelea kumuunga mkono Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutokana na kazi kubwa aliyofanya katika kupigania maendeleo ya Mtanzania.
Mang’o alisema kuwa Mama Samia ametengeneza fursa nyingi za kiuchumi ambazo wanawake wanaweza kuzitumia na kuimarisha uchumi wao kwa kufanya shughuli mbalimbali hivyo amewataka wanawake hao kutoka ndani na kwenda kuchangamkia fursa hizo.
0 Comments