Header Ads Widget

TUME YAUNDWA KUPITIA MAPENDEKEZO YA WANANCHI KUBADILI MATUMIZI YA ARDHI MALINYI



Mkuu wa wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba ameunda tume maalum na kuipa wiki tatu kukamilisha zoezi la kupitia eneo la ardhi la Ikerekere lililopo Kijiji cha Mabanda na kuishauri serikali kama iwaachie wananchi wa Kijiji hicho maamuzi ya kubadilisha matumizi na kuwa mashamba kutoka matumizi ya sasa ya kuwa eneo la malisho ya wafugaji.


Eneo hilo tangu mwaka 2003 lilikuwa likitumika na wafugaji kulishia mifugo yao kwa mujibu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Kijiji hicho.


 Ikumbukwe kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 wananchi katika vijiji wanayo mamlaka kupitia mikutano yao kuamua mabadiliko ya matumizi ya ardhi.Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya mwaka 1999 wananchi katika vijiji wanayo mamlaka kupitia mikutano yao kuamua mabadiliko ya matumizi ya ardhi.



Mkuu wa wilaya ameitaka tume hiyo kupitia eneo hilo na kujiridhisha kama eneo  linafaa kwa kilimo ili wananchi hao waachiwe maamuzi waliyoamua katika mkutano halali wa Kijiji uliokaa na kuamua kubadilisha matumizi yake.


Akizungumza na wananchi wa Kijiji hicho Mach 22, 2023,Waryuba ameunda tume ya watu watano ambao ni wataalamu kutoka halmashauri ya wilaya ya Malinyi na kutoka vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo na kutoa wiki tatu waishauri Serikali juu ya mabadiliko hayo ya ardhi.


Amewataja wajumbe wa tume hiyo kuwa ni Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Malinyi SSP Samweli Kijanga,Mkuu wa TAKUKURU wilayani Malinyi Sikujua Kimweri, Afisa kilimo wilaya ya Malinyi Martin Mhode, Afisa Maliasili na na hifadhi ya mazingira wilaya ya Malinyi Hamis Kitambuliho na Afisa Tarafa Ngoheranga Andrew Mgutwa.



Tume hiyo imeongezewa jamii za wakulima na wafugaji watano ambao ni wakazi wa Kijiji hicho ambapo watakuwa na kazi ya kupitia eneo hilo kufanya mikutano ya wananchi na hatimae kupitia muhtasari wa mkutano wa kijiji na kisha kuishauri serikali ya wilaya kabla ya kufanya maamuzi.


Wananchi waliojitokeza katika mkutano huo waliibua hoja hiyo ambapo waliitaka Serikali ya wilaya kuamua hatma ya katazo la kubadilisha matumizi ya ardhi ndani ya eneo tajwa ambapo wananchi waliungana na kumshauri mkuu wa wilaya kuwaachia eneo hilo kufanya kama eneo la kilimo.


Hoja hiyo haikupingwa na Mkuu wa Wilaya ambae aliwataka wananchi kuendelea na uvumilivu na kuiachia serikali kujiridhisha kuhusu maamuzi hayo na kisha itatoa maamuzi lakini akiwataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa tume aliyounda.



Aidha katika mkutano huo mkuu wa wilaya pia amewataka wafugaji na wakulima waliovamia katika mipaka ya pori la akiba la Kilombero kufahamu kuwa wanatakiwa kuhama kutokana na sheria iliyosainiwa na Mheshiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi February mwaka huu ambayo itawataka wavamizi kuondoka katika maeneo hayo.


Ametumia mkutano huo kusisitiza suala la utunzani wa mazingira ambapo amesema wajibu wa kila mwananchi na viongozi wao ni kutunza mazingira na kuhakikisha sheria ndogo za utunzaji wa mazingira zinaandaliwa na kupitiwa ili kuokoa ardhi chepe.



Mkuu wa wilaya ya Malinyi yupo katika ziara ya kikazi katika vijiji vya Wilaya ya Malinyi akijitambulisha na kutoa maelekezo na mwelekeo wa uongozi wake katika vijiji vya Wilaya hiyo ambapo Machi 22 amefanya mikutano katika vijiji vya Mabanda na Lupunga.


IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-H/W MALINYI


Na Prosper Kulita.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI