Header Ads Widget

TCCIA KIGOMA YAVUTIA WAWEKEZAJI KUTOKA INDIA

 


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

CHAMA Cha Wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo (TCCIA) kimewataka wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini India kuwekeza mkoani Kigoma kutokana na fursa nyingi za uwekezaji zilizopo mkoani humo.

Hayo yameelezwa kwenye kikao cha pamoja baina ya uongozi wa Chama hicho, Wafanyabiashara wa  mjini Kigoma na Balozi wa India nchini, Binaya Srikanta Pradhan kilichofanyika mjini Kigoma ambacho msingi Mkuu kikieleza fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo.



Mwenyekiti wa TCCIA mkoa Kigoma,Abdul Mwilima akizungumza mbele ya Balozi huyo wa India na Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa kikao hicho ni matokeo ya ziara ya viongozi na watendaji wa chama hicho wapatao 29 waliyoifanya nchini India Novemba mwaka jana.



Mwilima alisema kuwa ziara yao nchini India inatokana na ushirikiano wa kindugu uliopo baina ya Tanzania na India na kupitia TCCIA na chama cha wafanyabiashara wa India walipanga ziara hiyo kuona hali ya uwekezaji kuhusu kilimo, viwanda, biashara, utalii,huduma za afya na kuzungumza na wafanyabiashara ambao wataweza kuwekeza mkoani humo.



Mwenyekiti huyo alisema kuwa mkoa Kigoma unayo fursa kubwa ya uwekezaji kwenye kilimo, viwanda na usafirishaji kwani lipo soko kubwa la bidhaa za chakula na viwandani kwenye nchi za ukanda wa maziwa makuu ambapo una karibu watu milioni 25.



Akizungumza katika mkutano huo Balozi wa India alisema kuwa amefarijika kuona fursa kubwa ya uwekezaji iliyopo mkoani humo na kwamba tayari nchi hiyo inatekeleza mradi wa maji wilayani Kasulu wenye thamani ya shilingi Bilioni 2 ambao utaongeza chachu ya serikali ya India na wafanyabiashara wa nchi hiyo kuiweka mkoa Kigoma kwenye ramani yao ya uwekezaji na biashara.


Balozi huyo alisema kuwa India inafanya biashara kubwa na uwekezaji nchini Tanzania ambayo inakaribia  shilingi trilioni 15 hivyo kuwepo kwa fursa hiyo ya uwekezaji mkoani Kigoma kutaongeza thamani ya uwekezaji wa nchi hiyo kwa Tanzania.



Mkuu wa mkoa Kigoma,Thobias Andengenye alisema kuwa serikali imeuchagua mkoa Kigoma kuwa moja ya mikoa ya kimkakati katika ukuaji wa uchumi wa katika biashara na uwekezaji hivyo ipo miradi mbali mbali ambayo inatekelezwa kwa sasa mkoani humo.



Andengenye alisema kuwa mkoa umetenga maeneo ya uwekezaji ikiwemo eneo maalum la uwekezaji KISEZ, uboreshaji wa miundo mbinu ya barabara, reli, usafiri wa majini na viwanja vya ndege ili kuwezesha mkoa huo kufikika kwa urahisi.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI