TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imebaini mapungufu kwenye miradi ya maendeleo ya thamani ya shilingi bilioni 11.4 na kusema wahusika watachukuliwa hatua za kisheria baada ya uchunguzi kufanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha wakati akitoa taarifa ya kipindi cha robo ya Oktoba hadi Desemba 2022, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Christopher Myava alisema kuwa mapungufu hayo yamebaibika baada ya uchunguzi.
Myava alisema kuwa moja ya miradi hiyo ni Shule mpya ya Sekondari ya Viziwaziwa iliyopo Halmashauri ya Mji Kibaha yenye thamani ya shilingi milioni 470 ambapo imeezekwa kwa mabati ambayo hayana viwango vinavyotakiwa kuezeka majengo ya serikali.
"Mabati yaliyotumika kuezekea jengo la Utawala, maabara na vyoo vya shule hayakuwa na kiwango kilichothibitishwa kuezekea majengo ya serikali ambayo ni geji 28 badala yake yametumika ya geji 30,"alisema Myava.
Alisema kutokana na kubaini hayo uchunguzi unaendelea na hatua kali za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika kwa waliohusika na jambo hilo.
Aidha alisema kuwa mradi wa ukarabati wa skimu ya maji kwenye Kijiji cha Mkongo Wilaya ya Rufiji yenye thamani ya shilingi milioni 512.2 uchunguzi umebaini tanki moja la kuhifadhia maji linavujisha maji.
"Pia milango ya jengo la ofisi ya Jumuiya ya watumiaji maji Kijiji cha Mkongo haikuwekwa kwa ubora ambapo tumemtaka meneja wa Mamlaka ya Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA) kumwambia mkandarasi wa mradi ahakikishe mapungufu yaliyopo yanarekebishwa kabla ya muda wa matazamio kwisha,"alisema Myava.
Alibainisha kuwa kwenye uchambuzi wa mifumo kwenye uendeshaji na usimamizi wa masoko ya biashara na utekelezaji wa miradi kwa kutumia force account kwenye vyama vya ushirika vya msingi vya mazao na masoko (AMCOS) kuna udhaifu ikiwa ni pamoja na utunzaji wa kumbukumbu.
"Kwenye Amcos ya Kipo wamegundua udhaifu wa utunzaji nyaraka na kumbukumbu ambazo zinatunzwa nyumbani kwa viongozi wa bodi na kuharibiwa na mchwa hivyo kutokana na kuharibika kwa kumbukumbu hizo kunasababisha changamoto katika kubaini mapato na matumizi, takwimu na taarifa zote za fedha kwa ujumla,"alisema Myava.
Mwisho.
0 Comments