NA THABIT MADAI_ MATUKIO DAIMA APP-ZANZIBAR
TATIZO la Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia Visiwani Zanzibar bado linaripotiwa kuwepo kwa Asilimia kubwa licha ya Serikali na Taasisi binafsi kuwa na Jitihada mbalimbali katika kupambana nalo, tatizo hilo huwa ni chanzo cha Matatizo mengine katika Jamii.
Taarifa za Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia zinapo ripotiwa katika vyombo mbalimbali vya Habari zile zinazowahusu watoto wadogo huchukua nafasi kubwa ukilinganisha na Watu wazima.
Kwa Mujibu wa takwimu za mpango kazi wa taifa wa Zanzibar kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto wa mwaka 2017/2022, ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar, asilimia tisa ya watoto wa kiume na asilimia sita ya watoto wa kike visiwani humo hudhalilishwa kimwili na kingono wakiwa chini ya umri wa miaka 18.
Takwimu hizo zinaeleza kuwa kati ya watoto 10 waliokumbwa na udhalilishaji, mtoto mmoja ameripoti kwenye vyombo vya kisheria na kupatiwa huduma zinazostahiki huku ikionesha kuwa nusu ya watoto wa kike na wa kiume waliokutana na vitendo hivyo wamesimulia walichotendewa.
Makala hii imeangazia hali halisi ya matendo ya Udhalilishaji kwa Watoto Visiwani Zanzibar na Mapambano yanayofanyika katika kupunguza na kuondoa Matendo hayo ambayo yamekuwa yakitia doa linalochafua haiba ya Zanzibar.
*HALI HALISI*
Abeda Rashid Abdallah ni Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo Jinsia, Wazee na Watoto anaeleza kuwa hali bado hairidhishi licha ya kuwa na jitihada mbalimbali kwa wadau kwani Matukio yanaripotiwa kwa Wingi.
Alieleza kuwa kwa Mujibu wa Takwimu za Wizara hiyo zinaeleza kuwa kwa mwaka 2021 Jumla ya Matukio 1222 za Udhalilishaji kwa watoto yameripotiwa ambapo Matuko 846 yanawahusu watoto wa Kike.
Aliongeza kuwa kwa Mwaka 2022 kuanzia Januari hadi Agosti Matukio 598 yameripotiwa ya Udhalilishaji na Ukatiliwa kwa Watoto huku Matukio 396 yakiwahusu watoto wa Kike.
“Hali bado hairidhishi kutokana na kuripotiwa kwa matukio mengi na kwa mujibu wa Takwimu tulizozitoa kupita Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali jumla ya kesi 170 zimeripotiwa huku kesi zinazowahusu Wanawake 18 na Kesi 152 zinawahusu watoto,” Alisema.
Alifafanua kuwa katika Kesi hizo ambazo zimeripotiwa kwa Mwezi huo wa Septemba ni pamoja na Kesi za kutorosha, kubaka, Kulawiti, Shambulio la Aibu na mambo mengine yanayoendana na Ukatili wa Kijinsia.
“Takwimu hizi zinaonesha hali halisi ya Matukio haya hadi hivi sasa ambapo kesi nyingi zinaendelea kuripotiwa huku wahanga wakubwa wakiwa Watoto wadogo na Wanawake,” alisema.
*MIKAKATI YA SERIKALI*
Hata hivyo Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa Zanzibar jamii ina uwelewa Mkubwa juu ya Masuala ya Udhalilishaji na Ukatili na athari zake ambapo hupeleka Matukio mengi kuripotiwa.
“Tunamshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hssein Ali Mwinyi kwa kuanzisha Mahakama Maalum inayosikiliza kesi za Udhalilishaji ambapo kila siku kesi zinatajwa na kutolewa hukumu,”alisema.
Alifafanua kuwa Kesi nyingi huwa zinatajwa pamoja na hukumu yake jambo ambalo linaonesha kwa namna gani kesi zinavyoweza kufanya kazi zake.
Alisema, Serikali kupitia Wizara ya Wizara ya Maendeleo Jinsia, Wazee na Watoto inasimamia misingi ya Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali ambayo inaeleza nini kifanyike katika kuondoa kabisa suala la Udhalilishaji Visiwani Humo.
“Mbali ya kuwepo kwa Sera, Sheria na Miongozo kuna mahakama maalumu zimeanzishwa katika ngazi ya mikoa ili kuona Watu wanapata fursa za kutoa taarifa na mahakama zinachukua nafasi yake,” alisema.
Aliongeza kuwa, Hatua hiyo inasaidia katika kuona Serikali haijakaa kimya na kuonesha inajali haki za Watu hivyo kitendo cha Wananchi kuripoti kesi Mahakamani hadi kutolewa hukumu ni kitendo cha kuwajali Wananchi wake.
Mkurugenzi Abeda alieleza kuwa katika kupambana na Matendo hayo ya Udhalilishaji Wizara imeanzisha kuwa na Wasaidizi wa Sheria 70, Unguja 42 na Pemba 28 ambao wanatoa msaada wa Sheria kwa Wananchi walioshindwa kuripoti kesi na hata watu wa kuwasaidia kuwasimamia kesi zao.
“Hata hivyo Serikali ina Idara maalumu ya msaada wa Kisheria ambapo Idara hiyo ina wasaidizi wa Sheria zaidi ya 281 katika Maeneo mbalimbali Unguja na Pemba lengo ni kuona kwamba wa watu wanapata wasimamizi wa Sharia na Kesi zao zinakwenda mbele,” Alieleza.
Hata hivyo alifafanua, Serikali kupitia Wizara hiyo ina maafisa waratibu wa Wanawake na watoto Unguja na Pemba kwa lengo la kuibua na kuripoti matukio yote pamoja na kuwapa ushauri nasaha waathirika wa majanga hayo.
“Kwa hiyo hawa maafisa wanawake na watoto wa Unguja na Pemba katika Shehia zote kazi zao ni kusaidia angalu watu wetu waweze kupata auhuweni ya matukio hayo ambayo yanatokea takribani kila siku,” alieleza.
“Hata hivyo tuna viongozi wa Dini wapatao 88 Unguja na Pemba kazi yao ni kuwarusha watu katika Misingi ya kiimani ambapo huwa tunakutana nao hapa Wizarani kwa kila baada ya Miaezi mitatu na kutupa ripoti kwa kila ambacho kinaendelea,” aliongeza kueleza.
Katika nyingine Mkurugenzi huyo alieleza kwamba Serikali ipo katika hatua za kuanda mpango kazi mpya wa taifa wa kukabiliana na Vitendo vya Udhalilishaji mara baada ya Mpango kazi wa mwaka 2017 /2022 kupitwa na wakati.
Alieleza kuwa kwa sasa wapo katika hatua ya kupitia mpango ili kuona yale mapungufu yaliyopo kasha kuandaa mpango kazi mpya ambayo utaendana na hali halisi iliyopo hivi sasa.
0 Comments