Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MBUNGE wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru amewataka wakulima wadogo wa michikichi kwenye jimbo hilo kuongeza mashamba na kutumia ushauri wa wataalam kwani kilimo hicho kina nafasi kubwa ya kuwafanya wakulima hao kuondokana na umasikini.
Kavejuru alisema hayo akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Bukuba akiwa kwenye ziara ya kutembelea wapiga kura na kufanya mikutano kwenye vijiji mbalimbali vya jimbo hilo.
Mbunge huyo alisema kuwa serikali imeweka jitihada kubwa katika kufufua na kuliendeleza zao hilo ili kuhakikisha uzalishaji wa mafuta ya mawese unakuwa mkubwa kuweza kutosheleza soko la ndani hivyo ni fursa nzuri kwa wakulima kuitumia kuhakikisha mkakati huo unawanufaisha kiuchumi wakulima wadogo.
“Kwa sasa fursa kubwa ya wakulima ni kuongeza mashamba kwa kupanda mbegu bora za TENERA ambazo zinastawi kwa muda mfupi lakini zinatoa mafuta mengi na hiyo inakuja kuwafanya muondokane na mazoea ya kuendele na michikichi ya mbegu za zamani ambazo uzalishaji wake mdogo,”Alisema Mbunge huyo wa Buhigwe.
Kavejuru alisema kuwa wameishawishi serikali kuweka ruzuku katika mbegu za zao hilo ili zigawiwe bure kwa wakulima sambamba na kuiomba serikali kuweka ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa chikichi hivo fursa ya mafanikio kwa wananchi watakaolima zao hilo kwa kufuata ushauri wa wataalam watakuwa na mafanikio makubwa kiuchumi kwa siku za usoni.
Kuhusiana na suala la masoko alisema kuwa serikali inategemea kuwa mnunuzi mkubwa lakini hata sasa mahitaji ya mafuta ya mawese na bidhaa zitokanazo na michikichi ni kubwa hivyo wananchi wasiwe na hofu ya kupata hasara katika uwekezaji wao kwenye kilimo cha michikichi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Buhigwe,Venance Kigwinya akiungumza katika mkutano huo alisema kuwa halmashauri hiyo katika bajeti yake ya mwaka huu imetenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza zao la michikichi ili kuongeza idadi ya wakulima na kuongeza uzalishaji.
Kigwinya alisema kuwa kwa sasa ambapo serikali imeliweka zao la michikichi kuwa zao la kimkakati wananchi hawana budi kutumia fursa hizo kushiriki kwa karibu kulima zao hilo na kuongeza mashamba.
Baadhi ya wakulima walioongea wakati wa mkutano huo wa mbunge akiwemo Shekhe Khalid Athuman Mkulima na mkazi wa kijiji cha Bukuba wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma ambaye alisema kuwa upatikanaji wa mbegu mpya za michikichi na changamoto ya masoko ambayo wanunuzi wanawanyonya inawakatisha tama wakulima kuwekeza fedha zao kwenye zao hilo.
![]() |
Mashine ya kukamua mawese iliyopo kijiji cha Bukuba wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma |
Naye Hozea Bashima alisema kuwa bado upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya kilimo imekuwa changamoto kubwa na wengi wao bado wanalima mashamba madogo madogo yasiyozidi hekari mbili hivyo kuiomba halmashauri ya wilaya Buhigwe kuweka mazingira ya upatikanaji wa maeneo ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
0 Comments