Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Ili kuinua kiwango cha taaluma kinachokwamishwa na nidhamu duni ya baadhi ya wanafunzi katika shule za serikali hapa nchini mkuu wa mkoa wa Njombe amewaagiza wakuu wa shule kuwafukuza shule wanafunzi wote wanaokutwa na utovu wa nidhamu.
Mbele ya mkuu wa Mkoa wa Njombe aliyezuru katika shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu iliyopo Matembwe wilayani Njombe Mkuu wa shule hiyo mwalimu Advera Bagoka amesema kuna baadhi ya wanafunzi wamekuwa na utovu wa nidhamu wawapo shuleni hapo jambo ambalo linawapa wakati mgumu kuwasimamia.
Changamoto hizo zinamuinua mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka na kutoa agizo la kuwafukuza shule wanafunzi wote wanaoshindwa kutii mamlaka na sheria za shule.
Aidha mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Sharifa Nabalang'anya amewataka wanafunzi hao kuacha visingizio vinavyoweza kukatisha ndoto zao na hivyo wanapaswa kusoma kwa bidii.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu akiwemo Namsifu Ngasa pamoja na walimu wameeleza changamoto mbalimbali zinazowakumba katika shule hiyo ikiwemo upungufu wa vyoo,uzio na adha ya maji.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli ameahidi kwenda kushughulikia changamoto hizo na kwamba tayari baadhi yake fedha zimeshatengwa.
Shule ya sekondari ya wasichana Manyunyu ina zaidi ya wanafunzi 700 na walimu wanaopindukia 40.
0 Comments