Header Ads Widget

MBUNGE WA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI ATEMBELEA TAASISI YA UUGUZI YA KUMBUKUMBU YA ZAWADI KATIKA KATA YA KIMOCHI.



Na WILLIUM PAUL, MOSHI.


MBUNGE wa Jimbo la Moshi vijijini, Profesa Patrick Ndakidemi amewataka wanafunzi wa chuo cha Wauguzi na Wakunga cha Zawadi Memorial Health Training Institute kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao za kuajiriwa au kujiajiri wenyewe. 


Prof. Ndakidemi alitoa kauli hiyo jana alipotembelea chuoni hapo kilichopo kijiji cha Sango kata ya Kimochi  kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika chuoni hapo.



Wakisoma risala yao, viongozi wa chuo walimweleza Mbunge kuwa chuo kina mafanikio mazuri kwani wanafunzi wote waliofanya mitihani ya kitaifa wamefaulu.  

Walieleza baadhi ya changamoto kubwa zinazowakabili ni Uhaba wa wanafunzi, Ufinyu wa ardhi, Umeme kukatika mara kwa mara, Uhaba wa maji ya Bomba, Miundombinu mibovu ya barabara ya kuelekea Chuoni, kushindwa kupata Hati Miliki ya eneo la Chuo na Ukosefu wa bweni la wavulana.



Walisema kuwa chuo kina mipango ya kuongeza kozi za stashahada ya Clinical Medicine, Medical Laboratory  na Pharmacy.


Akizungumza katika ziara hiyo, Ndakidemi aliushukuru uongozi wa Chuo kwa kumwalika kuja kujionea yanayoendelea chuoni hapo na kuwaahidi viongozi na wanafunzi hao kuwa atazishughulikia changamoto zilizopo kwenye uwezo wake na atasaidia kutangaza mambo mazuri aliyoyaona katika chuo hicho. 



Mbunge amewahakikishia kuwa yupo pamoja nao na watakapoendelea na ujenzi wasisite kumuita ili ashiriki kikamilifu kuandika historia katika chuo hicho.

Aidha Prof. Ndakidemi aliwaahidi kuwa balozi wa kukitangaza chuo kila itakapojitokeza fursa ambapo chuo hicho kinatoa stashahada ya Uuguzi na Ukunga ambapo kimesajiliwa na mamlaka zote husika hapa nchini na wahitimu wanatambuliwa na mamlaka zote za serikali. 


Kimesajiliwa na mabaraza ya Taifa ya Uuguzi na Ukunga (TNMC) na lile la Elimu ya Ufundi na Mafunzo (NACTE).



Akitoa shukrani zake Mkurugenzi wa Chuo hicho, Valeria Dominiki Mrema alimshukuru Mbunge kwa kuwatembelea na kumuomba Mbunge awe mlezi wa chuo hicho ambapo alikubali.

Mwisho..

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI