Header Ads Widget

LEMA ASHANGAZWA NA WANAOPINGANA NA KAULI YAKE INAYOSEMA BODABODA SIO AJIRA.

 


Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP Tnga.


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema) kanda ya Kaskazini Godbless Lema ameshangazwa na baadhi ya viongozi wanaomtaka afute kauli yake ya kudai kazi ya bodaboda inaleta umasiki na ufukara na ni laana badala ya kazi hiyo kuwa ni baraka.


Hayo ameyabainisha kwenye Mkutano wake wa hadhara uliofanyika Jijini Tanga ambapo alisisitiza kutokufuta kauli yake hiyo na zaidi amesisitiza kuwa Watanzania wanazidi kuwa masikini kutokana na kuifanya kazi ya bodaboda ndio maisha yao.


Aidha alisema baada ya kutoa kauli hiyo katika Mkutano wake wa hadhara Jijini Arusha baada ya kuwasili toka ughaibuni viongozi wengi wa Serikali na wasio wa kiserikali walitoa matamko na wengi walikwenda mbali wakidai wataandamana Nchi nzima kushindikiza kufutwa kwa kauli hiyo iliyowahusu bodaboda. 



Lema alisema ni jambo la ajabu kwa Serikali badala ya kutafakari hoja ya msingi kwa vijana hao ambao wanaathirika na kazi hiyo badala yake wanajaribu kupinga kwa nguvu bila ya kufikiri mustakabali wa vijana hao kwa miaka ijayo.


"Nilishangaa kumsikia mtu mmoja hapa Tanga anatoa tamko kuwa wao ni madereva wa bodaboda wanamaisha na wanaishi vizuri na wanamtaka Lema afute kauli yake! leo naongeza bodaboda sio ajira "Alisema Lema.


Mwenyekiti huyo alisema Serikali inawadanganya vijana na imeshindwa kuimarisha kilimo, biashara na kufufua uchumi wa Tanga ambapo Mkoa huu ulikuwa wa pili kwa viwanda,ardhi yenye rutuba kwa kilimo,bahari na bandari vijana wasingekuwa na haja ya kuwa bodaboda wangefanya kazi ambazo zinawaruhusu kukopesheka na baadhi yao wangejiajiri katika kilimo cha kisasa. Leo vijana wote kazi yao ni bodaboda na hawajui athari yake kwa miaka ijayo ambapo wanaweza kuathirika macho,mgongo,kifua na hata maradhi ya homa ya mapafu kitu ambacho ni hatari kwa vijana ambao ndio tegemeo kwa Taifa la kesho.


Vipi miaka 30 ijayo kwa kizazi cha famillia ambazo baba ni bodaboda kitakuaje umasikini umekuwa mkubwa na kusababisha wazazi kukosa muda wa kuangalia watoto ni hatari na Serikali imekaa kimya bila kutafuta njia sahihi ya kulisaidia kundi hili linaloangamia bila ya kujitambua.



"Wakati nashuka uwanja wa ndege Arusha nilipokelewa na bodaboda zaidi ya 300 nilitokwa na.machozi Mama yangu aliniuliza shida nini nikamwambia ndugu zangu hawanakazi na wanaumia na kazi hii ya bodaboda ambayo haina dhamana na maisha yao"Alisema Lema.


Lema yupo Tanga kwa ziara ya siku mbili iliyo na lengo la kukiimarisha Chama Mkoani hapa ambapo ameambatana na viongozi wa Kanda ya Kaskazini inayoundwa na Mikoa minne ambayo ni Arusha,Manyara,Kilimanjaro na Tanga.


Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti Kanda ya Kaskazini Yosepher Komba alisema wananchi wa Tanga bado hawajanufaika na viongozi wanaoteuliwa kwa maslahi ya kuufanya Mkoa huu kuwa kinara wa maendeleo na kuzalisha ajira kwa vijana ambao wengi wao wanaishi katika mazingira magumu.


Komba alisema Tanga ni Mkoa ambao umebarikiwa kwa kila nyanja ambapo Serikali ingeweka nguvu na kutumia vena rasilimali zilizopo Mkoa huu ungezalisha ajira nyingi na kuufanya kuwa kimbilio la vinaja wengi wasio na kazi Nchini kama ilivyokuwa kwa miaka ya zamani.


Nae Abdul Kambaya ambae alikuwa kiongozi mwandamizi toka Chama cha wanachi CUF aliyejiunga na Chadema alisema tatizo la Nchi hii ni mfumo na sio la viongozi wanaotawala.



Kambaya alisema ikiwa kutakuwepo na mfumo bora utakaoletwa na katiba mpya hakika mambo mengi yatabadilika kutokana na mtawala atalazimika afuate katiba bora inayomuongoza badala ya kuongoza Nchi kwa matakwa yake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI