Amon Mtega,_Nyasa
WANANCHI 88 waliopo kwenye mpango wa Tasaf katika Kijiji cha Lukali na Litumbakuhamba kata ya Linga Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wamelalamikia kukosa malipo yao takribani madirisha mawili ambayo sawa na miezi minne jambo ambalo limewapelekea kuingiwa na hofu ya kutokulipwa fedha hizo.
Akizungumza mwenyekiti wa Kijiji cha Lukali Sixbert Ndomba amesema kuwa katika Kijiji hicho wanufaika 56 katika kipindi cha madisha hayo hawajalipwa malipo hayo huku watendaji husika hawajatoa ufafanuzi wa kutosha kuhusu changamoto hiyo ambayo inadaiwa imekuwa kelo kwenye Kijiji hicho.
Naye mwenyekiti wa Kijiji cha Litumbakuhamba Felicks Mbunda amesema kuwa katika Kijiji anachokiongoza yeye wanufaika 32 wamekosa malipo ya Tasaf na kufanya jumla ya wanufaika 88 wa Vijiji hivyo viwili kukosa malipo yao.
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa mpango huo John Ngonyani wa Kijiji cha Lukali amesema kuwa walishangaa kuambiwa wao wasubiri malipo yao kuwa kulikuwa na matatizo ya kimfumo huku wakiwa wamesainishwa kwenye fomu za malipo.
Ngonyani amesema kuwa walipojaribu kuhoji wamedai kuwa wamekuwa wakijibiwa Lugha za kejeli kutoka kwa wahusika Lugha ambazo zimekuwa siyo rafiki kwa watu waliyoibuliwa kutoka kwenye kaya masikini.
Hata hivyo mkurugenzi wa Wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo amesema kuwa kulifanyika makosa wakati wa ulipaji wa awali kuwa baadhi ya wanufaika zaidi ya 200 katika Wilaya hiyo mfumo ulidaiwa kuwa ulikosea uliwalipa mara mbili (Dabo) na kuambiwa kuwa dirisha linalofuata wanufaika hao wasipatiwe malipo hadi mfumo utakapo wekwa sawa.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa kila mnufaika atapatiwa malipo yake pindi mfumo ukiwa tayari na kuwa hakuna ambaye yupo kwenye mpango akakosa kupatiwa malipo yao ,huku akiwaomba wawe na subira.
Kwa upande wa baadhi ya watumishi kutoa Lugha mbovu kwa wanufaika hao atalifuatilia na akibainika atachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa Serikali iliweka mpango huo kwa lengo la kumuinua kiuchumi mwananchi na siyo vinginevyo .
Pia Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Ruvuma Xsaveria Mlimira amesema ni kweli kulitokea changamoto za kifumo kutoka makao makuu hivyo walipatiwa maelekezo na kuwa wote watalipwa malipo yao yote kwenye dirisha linalofuata.
Akizungumzia suala la utoaji wa Lugha mbovu kwa wanufaika mratibu huyo amesema kuwa alishatoa maelekezo kwa wakurugenzi wote kwa barua kuhakikisha wanawadhibiti watu wao katika matumizi ya Lugha dhidi ya wanufaika.
0 Comments