Header Ads Widget

TASAC YAANZA MCHAKATO UJENZI VITUO VYA UOKOZI, MELI KWENYE MAZIWA MKUU NCHINI

 




Na Fadhili Abdallah,Kigoma

SHIRIKA la uwakala wa meli nchini (TASAC) limeanza mchakato wa ujenzi wa vituo vinane vya uokoaji katika maziwa makubwa matatu nchini sambamba na ununuzi wa boti nne ambazo zitatumika kwenye zoezi la uokoaji kwenye maziwa hayo.



Mwenyekiti wa bodi ya TASAC,Kapteni Mussa Mandia amesema hayo wakati wa majumuisho ya ziara ya wajumbe wa bodi hiyo mkoani Kigoma kutembelea bandari za mkoa huo kuona hali ya usimamizi wa udhibiti wa usalama wa vyombo vya usafiri na usafirishaji majini mkoani humo.



Mandia alisema kuwa taratibu za utekelezaji wa mpango zimeshaanza ikiwemo kutambua maeneo ambaayo kutajengwa vituo hivyo ambapo alibainisha kuwa  kwa ziwa Victoria kutakuwa na vituo sita sambamba na boti mbili ziendazo kasi, ziwa Nyasa kituo kimoja na boti moja.


Mwenyekiti huyo wa bodi ya TASAC alisema kuwa kwa mkoa Kigoma kwa sasa kutakuwa na kituo kimoja cha uokoaji kitakachokuwa Kigoma mjini na boti moja iendayo kasi ambapo tayari eneo la ujenzi wa kituo hicho limepatikana lililopo Bangwe manispaa ya Kigoma Ujiji.



“Katika mwomgozo wa serikali wa kamati ya maafa na maelekezo yaliyotolewa utekelezaji wake ndiyo unaanza na kwa sasa tunatafuta mzabuni ambaye atapewa kazi ya ununuzi wa boti hizo nne na mipango mingine ya ujenzi wa vituo hivyo vya uokoaji inaendelea,”alisema Kapteni Mandia.



Pamoja na hivyo Mwenyekiti huyo alisema kuwa kamati za usimamizi za rasilimali za pwani (BMU) kwenye maziwa hayo  kwenye vijiji mbalimbali vilivyopo mwambao wa maziwa hayo zitaendelea kutumika kwa kupewa mafunzo ya uokoaji ili kuweza kutoa huduma ya haraka ajali zinapotokea wakati msaada wa vituo hivyo utakapokuwa unaelekea eneo la tukio.


Wakizungumzia ujenzi wa vituo hivyo wadau wa usafirishaji majini katika ziwa Tanganyika mkoani Kigoma wamesema kuwa kituo cha uokoaji kwa ajili ya vyombo vya majini ni muhimu kwani wamekuwa wakipoteza mali zao na maisha ya watu kwa kukosa msaada wa uokozi kutokana na kutokuwepo kwa vyombo vinavyoweza kutoa msaada wa haraka.


Mahmoud Jarufu kutoka Umoja wa wamiliki wa maboti mkoa Kigoma (UWAMAKI) alisema kuwa wamiliki na wasafirishaji wa shehena na abiria kwenye ziwa hilo wamekuwa wakipata hasara kwa kutokuwa na vyombo madhubuti na watu wenye mafunzo kwa ajili ya uokoaji ajali zinapotokea hivyo ujenzi wa vituo hivyo ni faraja kubwa kwao.


Naye mmiliki wa meli ya mizigo kwenye ziwa Tanganyika mkoani Kigoma,Mbaraka Mussa alisema kuwa kituo cha uokoaji ambacho TASAC imetangaza kuwa kitajengwa Kigoma na faraja kubwa sana kwao kwani hakuna taratibu zozote zilizopo zaidi ya wenye maboti na wavuvi ndiyo wanaosaidia yanapotokea majanga.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI