Header Ads Widget

TARURA WASISITIZWA KUTOPOKEA MIRADI YA BARABARA ITAKAYOJENGWA CHINI YA KIWANGO

 



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki (Mb), amewaelekeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi wanaojenga barabara ili ziwe na ubora wa hali ya juu na kuzisimamia kwa umakini pamoja na kuzifanyia ukaguzi wa mara kwa mara.


Mhe. Kairuki ameyasema hayo alipokutana na Bodi ya Ushauri ya TARURA, Menejimenti, Mameneja wa Mikoa na Wilaya pamoja na watumishi wa TARURA katika kikao kazi cha kupokea taarifa za kiutendaji za Wakala kilichofanyika jijini Dodoma.


“Tukumbuke ubora wa barabara zetu, hatutengenezi sisi ni Makandarasi lakini tuhakikishe kwanza barabara zetu hizo zina ubora wa hali ya juu lakini zinasimamiwa kwa umakini mkubwa na kukaguliwa mara kwa mara”, alisema Mhe. Waziri.



Aidha, Mhe. Kairuki amewataka TARURA kutopokea barabara ambazo hazijakidhi viwango kulingana na mikataba waliyoingia na Makandarasi na kutosita kuchukua hatua kulingana na mkataba kwa maeneo ambayo yameleta shida kama ambavyo mikataba na sheria zinavyowaelekeza.


Waziri Kairuki amehitimisha ziara yake ya siku mbili ambapo siku ya kwanza alifanya mkutano na Makatibu Tawala Wasaidizi Sekretarieti za Mikoa (Miundombinu), Wakuu wa Idara za Miundombinu na Maendeleo ya Vijijini na Mijini katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mameneja wa TARURA Mikoa na Wilaya. Siku ya pili ametembelea ofisi za TARURA Makao Makuu na kufanya kikao kazi na Bodi ya Ushauri ya TARURA, Menejimenti, Mameneja Mikoa na Wilaya pamoja na watumishi wa TARURA.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI