Serikali mkoani Iringa kupitia Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA imetiliana saini na wakandarasi mbalimbali mikataba minne ya ujenzi wa miradi ya maji yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.6 ambayo baada ya kukamilika kwake inatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya elfu 12 na kuongeza upatikanaji wa maji mkoani humo kwa asilimia 1.2.
Kufungwa kwa mikataba ya Miradi hiyo kunakuja baada ya jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha Tanzania inamaliza tatizo la maji ifikapo mwaka 2025.
Hata hivyo, wakandarasi hao, kupitia maandishi wameahidi kukamilisha miradi hiyo mapema iwezekanavyo na kuifanya iringa kukamilisha miradi ya maji kabla ya muda tarajiwa.
Naye Mkuu wa mkoa wa Iringa Mheshimiwa Halima Omar Dendego amesema kuwa ataendelea na kasi iliyopo ili aweze kumaliza miradi yote kwa muda mfupi.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kalenga Mheshimiwa Jackson Gideon amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maji nchini kwani ndilo tatizo kubwa kwa Mtanzania.
Naye Mbunge wa viti maalum jimbo la Iringa mjini Ritha Kabati amesema kuwa kukamilika kwa miradi hii kutamtua mama ndoo kichwani ikiwa ni utekelezaji wa dhana hiyo kwa vitendo tofauti na miaka mingine.
Awali akitoa muhtasari wa mikataba Meneja wa RUWASA mkoa wa Iringa Mheshimiwa Joyce Bahati amesema kwa mwaka 2022/2023, mkoa wa Iringa ulitengewa Bilioni 10.562 ambazo zitasaidia ujenzi uendelezaji wa miradi 24 ya maji na kuongeza upatikanaji wa maji kutoka 74.57% hadi 81%.
0 Comments