Header Ads Widget

RC TANGA -AWAONYA WATAKOTUMIA VIBAYA VYANDARUA VYA MSAADA


Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP Tanga. 

Wananchi Mkoani Tanga wametakiwa kuacha kutumia vyandarua vya msaada kwa shughuli za ufugaji wa kuku na kuvulia samaki na atakaebainika anakwenda kinyume na matuzi ya vyandarua hivyo sheria kali zitachukuliwa dhidi yake.


Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi vilivyotolewa na Bohari ya madawa Nchini (msd) Mkoani wa Tanga.


Kufuatia tabia hiyo ya matumizi mabaya ya vyandarua hivyo amewaagiza viongozi wa Kiserikali,dini na kijamii kusimamia matumizi sahihi ya vyandarua hivyo vinavyogawiwa kwa wanafunzi hao na wananchi waelimishwe umuhimu wa matumizi sahihi ili kuepuka matumizi yasiotarajiwa.


"Lazima sisi viongozi tusimamie matumizi sahihi,ipo tabia kwa baadhi ya wananchi wanavitumia vibaya vyandarua hivi na sio malengo yaliyokusudiwa lazima tuchukue hatua kali"Alisema Mgumba.


Mgumba alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI imeandaa zoezi la kugawa vyandarua vyenye viuatilifu kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa Mikoa mitano ikiwemo Mkoa wa Tanga ili kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya malaria kinapungua hadi kufikia asilimia 0 ifikapo 2030.


Aidha alisema kiwango cha ugonjwa wa Malaria katika  mkoa wa Tanga ni asilimia 12.4% tofauti na Mikoa mingine hivyo ipo haja ya kuchukuliwa kwa hatua za makusudi za kudhibiti na kuutokomeza kabisa.


Kwa upande wake Meneja wa Bohari ya madawa Mkoani Tanga (msd)Sitti Abdurahman alisema zoezi la ugawaji wa vyandarua hivyo umezingatia mahitaji ya maeneo husika na vimetolewa vyandarua 529,641 kwa ajili ya shule 1,083 za Mkoa mzima wa Tanga.


Alisema Tanga ni kati ya Mikoa mitano iyofaidika na zoezi hilo ikifuatiwa na Mikoa ya Dodoma,Manyara, Iringa na Kilimanjaro ambapo imeingizwa katika mfumo wa kupunguza kiwango cha ugonjwa wa Malaria.


Sitti alisema  vyandarua hivyo vinathamani ya zaidi ya Shs Bil 2 na vitagawiwa kwa wanafunzi wote wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba bila ya gharama yoyote ili kutimiza lengo la Serikali la mpango wa Kitaifa wa kudhibiti Malaria.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI