Header Ads Widget

POSHO YA KUJIKIMU YA WANAFUNZI ELIMU YA JUU KUPANDISHWA HADI ELFU 10

 



Na WyEST_Dodoma


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupandisha posho ya kujikimu ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia Sh. Elfu kumi kwa siku.


Rais Samia amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wawakilishi wa Jumuiya za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania TAHLISO na ZAHILFE katika viwanja vya Ikulu Chamwino jijini Dodoma.


Aidha amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuinua elimu ya juu kwa kuongeza fursa za upatikanaji wake ikiwemo kuongeza wigo wa mikopo na kuwataka kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo ili iwanufaishe na wengine.



“Labda niwaambie tumekamilisha mkataba na Benki ya NMB wa thamani ya Sh. Bilioni 200 ili wazazi ambao mishahara yao inapita benki waweze kukopa kwa ajili ya vijana wao," amesema Rais Samia. 


Dkt. Samia amewataka wanafunzi kuwa na ufahamu kuhusu mwelekeo wa nchi na aina ya Taifa tunalotaka kulijenga ambalo litajitegemea kiuchumi huku akiwasisitiza kuweka mkazo katika masomo na kujiepusha na vitendo viovu. 


Mhe. Samia ameupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu kwa namna unavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa wakati.



"Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu na Timu yote ya Wizara kwa kazi nzuri sana mnayoifanya kuwahudumia watoto hawa na mipango mingi ambayo nimeiagiza Prof. Mkenda na timu yake wameibeba na kwenda kuitekeleza vizuri sana tena kwa muda mfupi. Zamani ilizoeleka unaagiza inakwenda kutekelezeka kwa muda mrefu ukiuliza unaambiwa fedha lakini sasa hivi ukiagiza linafanyika, tunasonga mbele," amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.



Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fursa ya kukutana na Wawakilishi hao na kumshukuru kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu ambapo alipoingia madarakani ameongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka TZS bilioni 464 hadi kufikia bilioni 654.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS