Header Ads Widget

MBUNGE ZUENA AENDELEA KUCHANJA MBUGA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI MKOANI KILIMANJARO.



NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


MBUNGE wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amevitaka vikundi vya Wakinamama ambavyo vilipewa fedha za mikopo ya Halmashauri mkoani hapo kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wananchi wengine.



Zuena alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na wananchi wa kata ya Mabogini wilayani Moshi ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi ili zipatiwe ufumbuzi.



Alisema kuwa, Rais Dkt Samia Suluhu Hasani kwa kuonyesha jinsi anavyowajali wananchi aliamua kila Halmashauri kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni vijana, Wakinamama na watu wenyeulemavu.



"Keki hii ya Rais Dkt Samia inapaswa kumnufaisha kila mmoja hivyo kwa vikundi ambavyo mlishapata keki hii niwaombe mrejeshe ili iweze kunufaisha watu wengine ambao hawajapata" alisema Mbunge Zuena.



Aidha Mbunge huyo alitumia pia nafasi hiyo kuwaasa Wakinamama wa kata ya madogini kuhakikisha wanaunga na kuunda vikundi ambavyo vitasajiliwa na kuanzisha miradi ili kuweza kupata mikopo hiyo ambayo hutolewa na Halmashauri bila riba.



Pia aliwataka kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hasani kwa kazi kubwa na nzuri ambazo amekuwa akizifanya kwa maslahi mapana ya wananchi.



"Wakinamama Mwanamke mwenzetu Dkt Samia Suluhu Hasani amekuwa akifanya kazi kubwa na ya mfano ambapo amekuwa akitupambania kutuletea miradi mbalimbali sasa ni jukumu letu sisi kutoka kwenda kuzisemea kazi hizo kila mmoja ajue" alisema Mbunge Zuena.



Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Mabogini, Bibiana Massawe alitumia nafasi hiyo kumuomba Mbunge huyo kuhakikisha wanapata Afisa Maendeleo wa kata kwani kata hiyo haina mtumishi huyo.



"Vikundi vingi vya Wakinamama na vijana vinamalalamiko mengi lakini haya yote yanasababishwa na kumkosa Afisa Maendeleo wa kata yetu hali inayopelekea kuhudiwa na mtumishi wa kata ya Arusha chini jambo hili linapelekea vikundi vingi kukosa mikopa kutokana na kutokujua nini wanachopaswa kufanya" alisema Bibiana.

Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI