NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro, Profesa Patrick Ndakidemi amesema kuwa katika kipindi kifupi cha Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hasani miradi mingi ya maendeleo imetekeleza katika Jimbo hilo.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mabogini mara baada ya kushiriki katika sherehe ya kuzindua Halmashauri ya CCM kata ya Mabogini iliyofanyika katika kitongoji cha Remiti.
Alisema kuwa, yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Serikali ya awamu ya sita ambapo baadhi ya miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya wilaya Serikali imeshatoa shilingi bilion moja.
Miradi mingine ni ya ujenzi wa barabara ya Gatefonga - Mabogini - Kahe kwa kiwango cha changarawe (368 milioni), usambazaji wa maji katika kijiji cha Mserekia (500 milioni) na ujenzi wa madarasa 15 katika shule za sekondari za Mpirani na Mabogini (300 milioni).
Wakiongea katika mkutano huo, wananchi wa eneo la Remiti walimweleza mbunge kuwa, kero zao kubwa ni uhaba wa maji ya kunywa kwa baadhi ya kaya, ukosefu wa umeme, kutokuwepo na maeneo maalumu ya kulishia mifugo yao, josho la kuogesha mifugo na kero ya kukosekana kwa shule ya sekondari kwani watoto hutembea umbali mrefu kufuata elimu katika shule za sekondari Mpirani na Mabogini.
Akijibu hoja za wananchi hao, mheshimiwa mbunge aliahidi kuwa atafuatilia kero zote na atawaletea mrejesho.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mabogini Kinyaiya alimshukuru mbunge kwa kutenga muda na kushiriki katika uzinduzi wa Halmashauri ya CCM Kata ya Mabogini, na kuongea na wananchi.
0 Comments