Na Matukio DaimaApp Iringa
Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy amewataka Viongozi wa Serikali za mitaa kuanzia Watendaji wa Kata Kufanya Msako wa Wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaenda Shule wakamatwe. Akizungumza wakati akiongoza Mkutano wa Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Iringa (DCC) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mh Veronica Kessy amesema:-
"Wanafunzi wote wa kidato cha Kwanza wanaotakiwa kuripoti Shule, wakaripoti Shule na taarifa niikute mezani kwani muda umepita shule zimefunguliwa tarehe 9 mwezi wa kwanza mpaka leo hivi tunazungumza ni tarehe 15 mwezi wa pili, huyu mtoto ambaye hajaripoti shule mpaka leo tunategemea tupate matokeo mazuri kweli. Kwahiyo niliagiza ufanyike Msako, wazazi na walezi ambao watoto wao hawajaenda Shule wakamatwe"
Aliendelea kwa kuwauliza watendaji kata kama wameshaanza zoezi hilo na kuwataka watoe majibu na Maelezo.
Pia aliomba kupata ripoti ya Kinachoendelea kutoka kwa Afisa Elimu na kumtaka Katibu tawala wa Wilaya ya Iringa (DAS) kufanya usimamizi pamoja na Utekelezaji wa maagizo hayo.
"Wazazi wote ambao Watoto wao hawajaenda Shule wakamatwe, kuna tabia ya Watendaji kukaa na kuwatetea wazazi, ila nashukuru Kwasababu karibia kila Kata ina Polisi kata sasa hivi, mkafanye msako makawakamate mpaka mtoto aende shule vinginevyo awe na sababu tofauti labda kifo na kama ni mimba atwambie mimba hiyo ni ya nani, kama ameozesha ndo tunaenda naye moja kwa moja mahakamani, ifanyike hivyo hivyo kwa darasa la Kwanza na Awali kwani tuliweka makadirio ili tupate mrejesho wake tujue ni asilimia ngapi"
Mkuu wa wilaya ya Iringa Veronica Kessy alimaliza kwa kuwataka Viongozi kufuata Maelekezo yanayotolewa.
0 Comments