Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wananchi wa Kata ya Igima wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe wamelalamikia kuchelewa kujengwa kwa kituo cha Afya ili hali serikali ilitoa fedha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 270 ili zitumike kwenye ujenzi wa kituo hicho tangu mwaka jana.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Igima wakizungumza mara baada ya Kamati ya Huduma za Jamii ya Halmashauri ya Wanging’ombe kutembelea eneo la ujenzi wa kituo cha Afya kuona hali ya ujenzi wakazi hao akiwemo Adam Mlimbila na Leonard Ngole Mwenyekiti wa Kijiji cha Igima wamesema wanashindwa kufahamu kwanini ujenzi huo unasua sua wakati fedha zilishatolewa na serikali.
Hali hiyo ya kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa kituo cha Afya Kata Ya Igima unamuibua Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wanging’ombe Agnetha Mpangile akiwa na Kamati ya Huduma za Jamii kutoa siku 90 kituo hicho kiwe kimejengwa, huku kaimu Mtendaji wa Kata hiyo Godwin Swalle akijitetea juu ya suala hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii Halmashauri ya Wanging’ombe ambaye ni diwani wa kata ya Wangama Fredrick Mwalongo ameonesha kusikitishwa na ucheleweshwaji wa ujenzi wa kituo hicho ili hali maeneo mengine walishamaliza kujenga.
Nao baadhi ya mafundi waliopewa kazi ya kujenga kituo hicho akiwemo Mexon Njaligo wameelezea sababu za kusuasua kwa ujenzi wa kituo hicho kilichochimbwa msingi pekee na kwamba maji ndio kikwazo kikubwa kwao.
Victoria Mbiduka na Anna Madembwe ni madiwani ambao ni wajumbe wa kamati hiyo ambao nao wanaunga mkono maelekezo ya mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Tangu mwaka jana mwezi wa sita serikali ilitoa fedha hizo lakini cha kushangaza hadi sasa ujenzi huo upo katika hatua ya msingi ilihali kata nyingine zilishamaliza ujenzi wa vituo vyao vya afya.









0 Comments