Na. Jacob Kasiri - Mbarali
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka amekagua zoezi linaloendelea la uwekaji wa alama za mpaka wa GN. 28 na uthaminishaji wa mali za wananchi waliomo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha Januari 3, 2023 wilayani Mbarali.
Akiwa katika kijiji cha Iyala wilayani Mbarali ambapo zoezi la uthaminishaji linaendelea Katibu Mkuu huyo alisema, "Sisi kama wizara tunatambua na kuthamini kazi kubwa mnayoifanya kwa maslahi ya Taifa, hivyo tutajitahidi kwa kushirikiana na wizara nyingine kuhakikisha baada ya zoezi la uthaminishaji huu wananchi wanalipwa na kuondoka ili kuhitimisha zoezi hili.”
Katibu wa Kamati hiyo Yassin A. Sharif alisema, " Tafsiri ya mpaka imefanyika ili kuondoa taharuki na kujenga uelewa kwa wananchi ili zoezi la uwekaji wa alama za mpaka liwe shirikishi na kuleta tija. Mpaka sasa mawe 405 yameshawekwa kwa umbali wa mita 500 kwa mawe madogo na km 1 kwa mawe makubwa kwa urefu wa km 202.5 kati ya km 350 zinazotarajiwa kuwekwa mpaka.”
Zoezi hili linaenda sambamba na uchongaji wa Mkuza kutoka vijiji vya Kata ya Madibila hadi maeneo ya NARCO umbali wa km 177,. Mkuza huo ni mpana ukionyesha alama sahihi ya mpaka kuthibitisha ni maeneo yapi yaliyomo ndani ya hifadhi na yale yaliyo nje. Kufikia Disemba 3, 2022 jumla ya wananchi 2910 walishafanyiwa uthaminishaji wa mali zao na uchakataji wa taarifa kujua gharama halisi za fidia unaendelea.
Naye, Mkuu wa wilaya ya Mbarali Mhe. Reuben Mfune alieleza kuwa zoezi linaendelea vizuri na kutaja changamoto ya baadhi ya maeneo kung’olewa mawe na kukwanguliwa rangi na wananchi. Pia alimuomba Katibu Mkuu kuongea na Makatibu Wakuu wenzake ili zoezi hili lihusishe wizara nyingi zaidi,akitolea mfano watu wa bonde la maji kushiriki kikamilifu kusaidia kuondoa miundombinu inayochepusha maji tofauti na sasa zoezi hilo linatekelezwa na TANAPA na Idara ya Ardhi tu.
0 Comments