Header Ads Widget

ELIMU YA UANZISHWAJI WA PROGRAMU YA "TAKUKURU RAFIKI" YATOLEWA BUKOBA

 

NA TITUS MWOMBEKI, Matukio Daima App Kagera.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoani Kagera imeanza uelimishaji rasmi juu ya  programu maalumu ya TAKUKURU RAFIKI inayolenga kukuza uelewa kwa viongozi jinsi ya kuibua kero  zinazowakabili wananchi katika masuala mbalimbali ikiwemo miradi inayotekelezwa na serikali.


Akitoa maelezo kuhusu dhima na umuhimu wa  programu hiyo kwa viongozi wa Manispaa ya Bukoba wakiwemo madiwani wakiongoza na mstahiki Meya wa Manispaa ya Bukoba Gybosn Godson, Mkurugenzi, wakuu wa idara mbalimbali pamoja na watendaji, kamanda wa TAKUKURU Kagera, John Joseph amesema kuwa programu hiyo imeanzishwa kwa maagizo ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani ikiwa na lengo la kutanua wigo kwa kushirikiana na wadau katika kupambana na vitendo vya rushwa nchini.

"Kama mnavyofahamu vitendo vya rushwa vikiachiwa vikaendelea kwenye nchi yetu inawezekana utoaji wa huduma na ujenzi wa miradi ya maendeleo unaweza usifikie malengo yaliyokusudiwa ndiyo maana sasa serikali imeona ili kukuza ustawi wa jamii katika kushiriki kwenye mapambano dhidi ya  rushwa na kusimamia miradi yao ya maendeleo na shughuli za utoaji wa huduma tuje na hii programu mpya ya TAKUKURU RAFIKI"


"TAKUKURU RAFIKI imelenga kutanua wigo  kwa watu pamoja na wadau ambao wanaweza kupambana dhidi ya rushwa na wadau waliolengwa ni pamoja na viongozi wote wakisiasa,madiwani,watendaji wa kata,wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya, wananchi wa kawaida,wadau wa maendeleo, wafadhili pamoja na waandishi wa habari hii yote ni kuibua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao na kutafuta ufumbuzi jinsi ya kutatua kero hizo"


Amesisitiza kuwa katika kutekeleza programu hiyo wananchi katika kata watagawiwa fomu maalumu ambayo itawataka kujaza kero iliyokithiri katika eneo lake na itakuwa siri na baadaye kero zitachambuliwa na kuanza kushughulikiwa. 

Kwa upande wake mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba, Hamid Njovu ameipongeza TAKUKURU kwa kuja na programu hii ambayo ni rafiki  na shirikishi na kuahidi kuwa watashirikiana ipasavyo ili kutokomeza vitendo vya rushwa.


"Kupitia programu hii kuzuia mianya ya rushwa lakini pia inamshirikisha mwananchi katika kutoa vipaumbele anavyovitaka katika kata yake tunaweza kuwa tunapeleka miradi mingi na mizuri kwa wananchi wakati fulani kumbe wananchi wale ile miradi sio vipaumbele vyao hivyo basi niwaombe tushirikiane sote katika kuitekeleza programu hii kwani itaibua kero za wananchi nazo zitaweza kutatuliwa kwa urahisi" alisema Njovu.

Naye diwani wa kata ya Bakoba, Shabani Rashird ameiomba ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ikitekeleza kuanzia hatua za mwanzo hadi mwisho kwani itasaidia wananchi kuhoji pale ambapo wataona hapajaeleweka na kuibua vitendo vya ubadhirifu.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI