BENKI ya CRDB imesema kuwa itaendelea kuunga mkono sekta mbalimbali kwa kutoa mikopo ikiwemo kwenye mnyororo wa thamani kwenye Uvuvi.
Hayo yalisemwa Chalinze Wilayani Bagamoyo na Meneja wa CRDB tawi la Bagamoyo Jane Christopher alipokuwa akizungumza na Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya Madiwani
Christopher alisema kuwa wanawezesha kwenye mnyororo wa thamani wa Uvuvi ambapo riba ya mkopo ni asilimia tisa.
"Hadi sasa mikopo kwa sekta ya uvuvi imetolewa baadhi ya maeneo ikiwemo Zanzibar na Ziwa Victoria hivyo na wavuvi ndani ya Mkoa wa Pwani wanakaribishwa kukopa,"alisema Christopher.
Alisema kuwa benki yao inaendelea kuboresha huduma zake za mikopo mbalimbali ikiwemo ya uwekezaji na makundi mbalimbali na sekta mbalimbali za kiuchumi.
"Mpango ni kuingia kwenye mazao ya korosho na ufuta ambapo kwa mkoa wa Pwani ni mazao ambayo ni tegemeo kwa wananchi wa mkoa wa Pwani hivyo nao watanufaika na mikopo kwenye mazao hayo,"alisema Christopher.
Aidha alisema kuna mikopo ya nyumba kwa watumishi ambapo wameingia ubia na Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) ambao wana miradi ya nyumba ambapo moja ya mkataba wa nyumba waliouingia ni ule wa Mama Samia.
Alibainisha kuwa wanasaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na ukarabati wodi ya wanaume kwenye hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, ununuzi wa vitanda shule ya wasichana Kibaha na udhamini wa utalii Vikindu Mkuranga.
0 Comments