Header Ads Widget

ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA TABORA ATAKIWA KULIPA FIDIA MILIONI 80.

 Na Lucas Raphael,Tabora

Mahakama ya Mkoa wa Tabora imemtaka aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Elick Komanya Kitwala kulipa mdai wake Alex Ntonge kiasi cha Shilingi milioni 80 kutokana na vitendo vya udhalilishaji.

 

Hakimu wa mahakama ya mkoa wa Tabora Jovith Kato akitoa hukumu hiyo alisema kwamba mahakama imemuona mshitakiwa kuwa na hatia baada ya kufanya vitendo vya udhalilishaji.

 

Alisema kwamba mshitakiwa akiwa mkuu wa wilaya ya Tabora alitumia vibaya madaraka yake na kutumia vyombo vya dola alivyokuwa anataka kwa sababu alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi ya wilaya hiyo .

 

Alisema kwamba mahakama inaamini kwamba mshitakiwa alitumia nguvu kutawala kuliko busara jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa nchini huru kama Tanzania .

 

Komanya ambaye alienguliwa ukuu wa Wilaya na Rais Dokta Samia Suluhu Hassan juni 19/2021 ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya Madai fidia ya Shilingi milioni 140 kutokana na vitendo vya udhalilishaji alivyomfanyia Alex Ntonge januari 05/2021.

 

Katika shauri hili la Madai namba 04/2021 mdai  alitaka  alipwe nafuu ya shilingi milioni 80 kutokana na kuzuiwa uhuru wake, Milioni 30 kutokana na tendo la kukamatwa na kushitakiwa kwa nia ovu na shilingi milioni 30 kwa kudhalilishwa utu wake.

 

Ntonge kupitia kwa wakili wake Kelvin Kayaga alidai kuwa siku hiyo Komanya akiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora akiwa ameambatana na askari wa jeshi la polisi walifika nyumbani kwa mdai eneo la Ipuli na kumkamata na kisha kumdhalilisha.

 

Aliongeza kuwa Komamya akiwa na askali wawili wenye Bunduki aina ya Smg baada ya kumkamata walimdhalilisha mbele ya familia yake na majirani zake ikiwa ni pamoja na kumwamuru apige magoti barabarani.

 

Mahakama ya Mkoa mbele ya Hakimu Mkazi Jovith Katto imefikia hatua hiyo baada ya kumaliza kusikiliza mashahidi wa pande zote mbili ukiwemo wa mkuu wa polisi Wilaya ya Tabora SSP George ambaye alitwa kama shahidi wa mshitakiwa Kitwala Komanya.

 

Katika utetezi wake mbele ya hakimu Katto huku akiongozwa na wakili wa Kujitegemea Issa Mavulla, Komanya alidai kuwa amefunguliwa shauri hilo kwa nia ya kumkomoa na kumkomesha.

 

Kato ni Hakimu wa Tatu kusikiliza shauri hilo ambalo awali lilianza kusikilizwa na hakimu Sigwa Nzige lakini mdaiwa alimkataa ndipo likaamishiwa kwa hakimu mkazi mfawidhi wa Wilaya ya Tabora Demotrio Nyakunga ambaye pia hakuendelea nalo..

 

Komanya alikana kuhusika na tuhuma zinazomkabili za vitendo vya udhalilishaji dhidi ya Mdai Alex Ntonge wakati wa uongozi wake wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora.


Hata hivyo wakati hukumu hiyo ikitolewa mshitakiwa Elick Komanya Kitwala hakuwepo mahakamani hapo .

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS