Dkt, Rachel Nungu Meneja Mpango wa Mradi Magonjwa yasiyoambukiza kutoka chama Cha kisukari Tanzania (TDA)
NA CHAUSIKU SAID,
MATUKIO DAIMAAPP, MWANZA
Watoa huduma za afya ngazi Msingi Takribani 630 kupatiwa mafunzo namna ya kuielimisha jamii wanayo ihudumia jinsi ya kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuepuka athari zitokanazo na magonjwa hayo ikiwemo vifo.
Mafunzo yatakayotolewa Kwa siku tano Mkoani Mwanza yakishirikisha watoa huduma kutoka katika vituo vya afya vya Mwanza, Simiyu, Kagera,Geita na Mara chini ya Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chama cha Kisukari Tanzania (TDA)
Akitoa taarifa ya mafunzo, Mwenyekiti wa Wakufunzi Dkt. Mwanaada Kilima alisema, lengo la kuwajengea uwezo watoa huduma hao kuwawezesha kuelimisha jamii katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza huku serikali ikiwa imeandaa mpango mkakati wa tatu wa kitaifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa hayo.
Alisema mkakati huo unatekelezwa kwa kuzingatia vipaumbele vya mpango mkakati wa afya wa taifa wa mwaka 2021 hadi 2026 inayolenga kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya ili kuboresha kiwango cha huduma za kinga, tiba na huduma tengemano za magonjwa hayo kuanzia ngazi za jamii mpaka taifa
Alisema moja ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vya afya 600 kwa kuwapa mafunzo watoa huduma za afya juu ya utoaji huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na yanayolenga kuwafikia watoa huduma za afya msingi wapatao 3000 kutoka mikoa 26 kufikia Desemba 2023.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa alisema magonjwa hayo yanachangia vifo kwa takribani asilimia 33 na hali hiyo inazidi kuwa mbaya kadri miaka inavyopita.
"Miaka ya 80 hadi 90 hali haikuwa hivi sasa hivi inaongezeka miaka inavyoongezeka, sisi wakati tunasoma tulikuwa tunasema ni magonjwa ya ulaya na wenye pesa hatukutegemea hali itakuwa hivi katika nchi yetu hali inazidi kuwa mbaya hivyo serikali imeamua kuweka jitihada ili kwenda sambamba na kupunguza hali ilivyo sasa hivi" alisema Rutachunzibwa.
Alisema kwa sasa kumekuwa na uvumi mwingi ambao kila mtu anaongea lake hivyo wahudumu hao watumie elimu watakayoipata kutoa taarifa sahihi kwa wananchi ambao inakuza ni zaidi ya asilimia 80 wanaopata huduma katika vituo vyao .
Alisema wananchi wanapaswa kujengewa moyo wa kujitokeza kupima na kutambua afya zao, namna ya kukabiliana na magonjwa hayo na wanapokuwa kwenye vituo vyao wasikubali mgonjwa apite bila kumshawishi kupima ama kumpatia elimu kwa kutumia njia hiyo itawaokoa wengi .
Pia waendelee kuwaelimisha wananchi kuhusu kushughulisha mwili, lishe bora, kuacha kuvuta sigara na matumizi ya pombe wasione kigugumizi na wasiishie kwenye tiba bali wazungumze kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo majukwaa waeleze madhara ya kutumia vitu hatari na wajenge mahusiano na viongozi mbalimbali wakiwemo wa vijiji na kata walizotoka.
Naye Kaimu Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt.Pius Kagoma, alisema lengo la serikali ni kuboresha ubora wa huduma ili kuyafikia maboresho hayo lazima wayaangazie magonjwa hayo ambayo mara nyingi yanaleta shida kubwa kwenye mifumo yao ya afya, imani yao watumishi hao wataisambaza elimu hiyo waliyoipata kwa watumishi wengine na huduma zitakuwa bora kwa wananchi .
Aidha Kaimu Meneja Mpango wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya Shadrack Buswelu, alisema lengo lao ni kuboresha huduma za afya kuanzia ngazi za msingi ili kuwa na vituo bora huduma nzuri ni vyema kuimarisha rasimali watu ambayo ni nyenzo muhimu kuhakikisha kuwa wanaimarisha huduma zao sambamba na miundombinu .
"Ukiangalia takwimu za vifo nchini magonjwa yasiyoambukiza yanachangia takribani asilimia 33 hiki ni kiwango kikubwa mno na kesi nyingi zinaeleza kumekuwa na tatizo la watoto kufa kabla ya kufikia miaka 70 kama wasipochukua hatua leo hili janga litatukuta hadi sisi na watu wengi watamalizika kwenye jamii bila kupata huduma kwa hiyo haya mafunzo kwetu ni muhimu sana kwa sababu wataenda kutoa huduma zilizobora kwa wananchi" alisema Buswelu.
Meneja Mpango wa Mradi wa Magonjwa yasiyoambukiza kutoka chama Cha kisukari Tanzania (TDA) Dkt, Rachel Nungu ameeleza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano, kutoa elimu pamoja na vifaa katika Mikoa yote iliyopata elimu ili kuweza kutambua magonjwa yasiyoambukiza na kuweza kuyaepuka.
"Lengo letu tunahitaji kuona magonjwa yasiyoambukiza yanapunguza kabsa katika Nchi yetu na tunaamini haya mafunzo yataleta mwamko Kwa washiriki pindi watakaporudi katika vituo vyao vya kazi" Alisema Dkt, Rachel.
0 Comments