Header Ads Widget

WANANCHI WA MTAA WA MWANZANGE JIJINI TANGA WAMUANGUKIA MKUU WA MKOA

Na Mbaruku Yusuph Matukio Daima APP Tanga.

Wananchi wa mtaa wa mwanzange kata ya Majengo Jijini Tanga wamemuangukia Mkuu wa Mkoa Tanga Omary Mgumba kuingilia kati mgogoro wa eneo la makazi wanayoishi na Taasisi ya Muslim Associations ya Jijini hapa ambayo wanadai eneo hilo ni la kwao.


Kauli hiyo imetolewa na Mjumbe wa Serikali za mtaa wa Mwanzange Regina Hatibu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa huyo alipotembelea eneo hilo kwa ajili ya kuzungumza na wananchi wanaoishi katika eneo hilo ili kubaini chanzo cha mgogoro huo.

Regina alisema mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa wazazi wao walikuwepo katika eneo hilo tangu mwaka 1930 na kufikia mwaka 1989 ndipo mgogoro ulianza baina yao na Taasisi hiyo inayodai eneo lote la hekari saba ni la kwao.


"Mkuu wa Mkoa tusaidie eneo hili ni kubwa lakini sio eneo lote ni la kwao eneo hili ambalo lina nyumba 21 ni la wakazi wa mtaa huu wa mwanzange tangu kipindi hicho cha wazee wetu" Alisema bi Regina.


Regina alisema kuwa ombi lao kwa Mkuu wa Mkoa ni kuachiwa kuendelea kuishi katika makazi hayo kwa kile wanachokiamini wana uhalali wa umiliki wa eneo hilo ingawa Taasisi hiyo imelifikisha jambo hilo mahakamani na kuamuliwa wananchi hao waondoke kwa kupewa notisi.

Aidha alisema baada ya mahakama kutoa maamuzi hayo ya ushindi kwa Taasisi hiyo walikata rufaa katika.mahakama ya Ardhi ambapo bado hakujatolewa maamuzi yoyote ingawa wanaishi kwa mashaka kutokana na hofu ya Kuja kuhamishwa.


Mzee Hamisi Hassan anaekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya Miaka 80 alisema wazazi wao waliishi katika eneo hilo tangu miaka ya 1930 na hapakuwa na mtu aliyejitokeza na.kudai eneo hilo ni mali yake.


Hassan amemwomba Mkuu wa Mkoa kufanya busara na kuwahurumia wananchi wa eneo hilo ambapo kama wataondolewa wanaweza wakawa na maisha magumu kwa kutokupata sehemu sahihi ya kuishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa alisema Serikali ipo pamoja na wananchi hao ingawa jambo hilo lipo mahakama ya Ardhi na kutokana na taratibu za Nchi Serikali haiwezi kuingilia chombo cha kisheria hadi pale kitakapotoa maamuzi yake.


Mgumba alisema lengo la ziara yake katika eneo hilo la hekari saba ambapo kuna sehemu ya makaburi,uwanja na makazi ya watu ni kuona namna gani wanaweza kukaa na pande hizo mbili Taasisi ya Ibadhi na wananchi hao kuona njia mbadala ya kumaliza mgogoro huo.


"Nimekuja kwa maelekezo ya Mh Rais kushughulikia jambo hili na sote tunajua kuwa mgogoro huu upo mahakamani na hatuwezi kuingilia tusubiri maamuzi ya kisheria ndipo tutakapoona namna ya kufanya"Alisema Mgumba.


Hata hivyo aliwatoa wasiwasi wananchi hao kwa kuwaeleza kuwa ipo njia ya mazungumzo inaweza kufanywa na Serikali pamoja na Tasisi hiyo nje ya makahama na kuumaliza mgogoro huo kwa kutumia busara.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI