NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR- MATUKIO DAIMA APP
WADAU wa Kupambana na Vitendo vya Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia Visiwani Zanzibar waungana pamoja kujadili na kutoa Mapendekezo katika Muongozo wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu wa Kuzuia na kudhibiti Ukatili wa Kijinsia Visiwani Humo.
Akifungua Mkutano wa siku mbili uliofanyika katika Ukumbi wa Jozani Mwanakwerekwe Mjini Unguja na kuwashirikisha wadau wa Taasisi za Serikali na Asasi za kiraia, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Mohammed Jabir alisema Mkutano unalenga kukusanya Maoni yatakayopelekea kutokomeza matendo hayo.
Alisema kuwa Muongozo huo ni wa Muda Mrefu tangu kutayarishwa hivyo Serikali imeona kuna haja ya kuwakutanisha wadau ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Muongozo huo na kutumika katika kukabilia na matendo ya Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia hususani Watoto na Watu wenye Ulemavu.
“Muongozo huu tangu kutayarishwa kwake ni muda mrefu hivyo kuna mambo hivi karibuni yameibuka ambayo kuna haja ya kuwepo katikza muongozo na Viongozi wa Dini kuweza kuutumia katika kukabiliana na Vitendo hivi,” alisema.
Aidha alieleza kuwa, Udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ni tatizo la kijamii hivyo wadau mbalimbali wanatakiwa kutoa mapendekezo yatakayopelekea kutokomeza matendo hayo.
“lengo la kukutana hapa kwa siku mbili ni kujadiliana kwa kina juu ya huu Muongozo wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu wa kuzuia na kudhibiti Ukatili wa Kijinisialengo likiwa ni kudhibiti matukio ya ukatili wa kijinsia yasiweze kuendelea kutokea na jamii yetu iweze kuishi bila ya kuwepo kwa kadhia hii,” alisema.
Mapema Mkuu wa Divisheni ya Kuratibu na Mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia Mulhat Hassan Ali alisema kuwa mkutano huo wa siku mbili ambao umelenga kuweka Masuala mtambuka katika mpambano ya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia.
Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar Sheikh Abdallah Twalib Abdallah amesema kuwa muongozo unaojadiliwa umepitwa na wakati kutokana kuwa ni wa muda mrefu na umeacha mambo mengi kutokana na hali ya sasa katika mapambano dhidi ya matendoi hayo.
“Ndani ya Miaka 10 tangu kuchapishwa kwa Muongozo huu kuna mambo mengi yamebadilika na matendo ya Udhalilishaji bado yappo na yanaripotiwa kwa Wingi,” alieleza.
Hata hivyo alisema kuwa, Muongozo huo uliacha kuzungumzia juu ya Watu wenye ulemavu hivyo ni vyema kwa wadau kutoa maoni yao ili kuboresha muongozo huo na kutumika katika khutba na darsa za viongozi wa Dini.
Mkutano huo wa Siku mbili wa kujadili na kutoa Mapendekezo juu ya Muongozo wa Viongozi wa Dini ya Kiislamu wa Kuzuia na kudhibiti Ukatili wa Kijinsia umeandaliwa na Divisheni ya Kuratibu na Mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji na Ukatili wa Kijinsia.
0 Comments