Header Ads Widget

UJENZI MADARAJA YA MAWE KUONGEZA UZALISHAJI MAZAO YA KILIMO BUHIGWE


 

Mbunge wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru (Mwenye suti nyeusi) akiongoza viongozi wa CCM wilaya Buhigwe na viongozi wa serikali  wa kata ya Janda wilaya Buhigwe  kukagua moja ya madaraja ya mawe yanayojengwa na Wakala wa barabara za mjini na Vijijini (TARURA) kuunganisha maeneo ya makazi ya wananchi na maeneo ya uzalishaji wa kilimo kurahisisha usafirishaji kuingia na kutoka kwenye maeneo hayo.


(Picha na Fadhili Abdallah)

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Na Fadhili Abdallah,Kigoma

MBUNGE wa jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma Felix Kavejuru amesema kuwa ujenzi wa madaraja ya mawe katika jimbo hilo kuelekea maeneo ya kilimo yatawezesha wilaya hiyo kuongeza maradufu uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kuwezesha sekta ya kilimo kuwa biashara.

Kavejuru alisema hayo alipofanya ukaguzi kwenye miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye jimbo hilo ikiwemo miradi ya madaraja ya mawe kwenda kwenye eneo la mashamba ya wananchi na kubainisha kuwa madaraja hayo yana tija kubwa katika kukifanya kilimo kuwa na tija.

Mbunge huyo alisema kuwa moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wakulima hao ni changamoto ya kuvuka mito mikubwa hasa wakati wa mvua nyingi kusafirisha mazao yao kutoka shambani kupeleka kwenye masoko ambapo kwa kukamilika kwa madaraja hayo kutaondoa changamoto hiyo.

Alisema kuwa hata wakati wa msimu wa kilimo wakati mwingine mvua zinapokuwa nyingi na mito kujaa ilisababisha wakulima kushindwa kuvuka kwenye mito hiyo kwenda mashambani na hivyo shughuli za shamba kukwama kwa siku kadhaa.

“Kwangu mimi naona ujenzi wa madaraja haya ambayo yamejengwa kwa ufadhili wa shirika la maendeleo la Ubeligiji (ENABEL) kupitia mradi wa maendeleo ya kilimo (SARKIP) utawezesha kuleta tija kubwa kwenye kilimo na kuongeza uchumi wa wakulima kwa kuzalisha kwa wingi na kuwa na gharama nafuu za kusafirisha mazao kutoka shamba kwenda kwenye masomo,”Alisema Kavejuru.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Janda, Stanley Ndoza alisema kuwa changamoto ya kutokuwepo kwa madaraja imara kulichangia kufifisha juhudi za wakulima katika kuongeza uzalishaji ambapo kwa sasa wakati madaraja hayo yakielekea kukamilika ongezeko la uzalishaji litakuwa kubwa na kukuza uchumi wa mwananchi mmmoja mmoja.

Ndoza alisema kuwa wakati wa masika baadhi ya mito ilikuwa haipitiki na iliwalazimu baadhi ya watu kulala mashambani au kupitia njia ndefu za mzunguko kutokana na mito kujaa ambayo mingine madaraja ya muda waliyokuwa wakijengwa yalikuwa yakibebwa na maji.

Mmoja wa wananchi wa kata ya Janda, Yoram Binza alisema kuwa miradi inayotekelezwa kwenye jimbo hilo imekuwa chachu kubwa kiuchumi ikiwemo madaraja ya mawe ambayo yamefungua njia za usafirishaji kuingia na kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hilo wakati wote ambapo wakati wa mvua ilikuwa changamoto kubwa.

Meneja wa Wakala wa barabara za mjini na Vijijini (TARURA) mkoa Kigoma, Godwin Mpinzile alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha madaraja ya mawe  matatu yenye thamani ya shilingi milioni 175 yanatarajia kukamilishwa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS